Sunday 9 January 2011

KUJIENDELEZA, MAZOEZI NA KUINUA VYUMA -Sehemu ya Mwisho

Makala kadhaa zilizopita zimesisitiza sisi wananchi wenyewe kujiendeleza. Lengo la insha hizi ni kukumbusha wewe mwananchi kwamba huwezi kusonga mbele bila elimu na maarifa sahihi; kwamba maendeleo yanawezekana.
Jamii ya Marekani imejenga utamaduni huu uitwao Self Help. Ni utamaduni uliozalisha biashara ya vitabu, video, magazeti na vipindi mbalimbali vya runinga vinavyosisitiza mwananchi kujituma badala ya kutegemea uchawi, dini au imani nyingine peke yake. Lengo ni kuweka nguvu za kimaendeleo mikononi mwa mwanadamu. Kelele inayopigwa ndani ya utamaduni wa Kimarekani ni kuwa lolote linawezekana kwa anayejitahidi.

Ukiichunguza jamii hii utagundua ilivyojikita ndani ya makucha ya mauaji, maisha ya haraka na mashindano. Silika yake ni Ubinafsi. Je, ubinafsi ni kitu kizuri au kibaya? Inategemea unalionaje suala, kisaikolojia. Unaweza kuangalia Ubinafsi kwa macho aina mbili. Mambo makubwa duniani zamani na leo yamegunduliwa kwa jitihada za kibinafsi; ingawa haina maana wagunduzi walikuwa Wabinafsi. Ila pale ambapo wanadamu walipotumia nafasi zao za kazi, taaluma au uongozi kuangamiza wenzao ni ubinafsi ambao Bongo tumeukatia jina la Ufisadi.
Hivyo chagua.
Ubinafsi ninaouangalia hapa ni wakujiendeleza.
Leo utamaduni wa Kimarekani umeenea duniani na kujenga hisia kwamba tunaweza kuwa matajiri na maarufu mara moja; bila kazi au maarifa. Utamaduni huu uliozagaa sana miaka ishirini iliyopita umekatiwa jina la utandawazi na kati ya njia kuu zinazousambaza ni mtandao, mawasiliano ya simu za mkononi na runinga. Tunaishi kipindi cha utandawazi na baadhi yetu tumefikia hatua ya kujidanganya kuwa kila kitu inawezekana bila jasho.
Katika nchi zilizoendelea vipindi vya runinga vimetengenezwa kuwapa washindi wasiokuwa na taaluma umaarufu na utajiri wa haraka haraka.
Tatizo la tunaoishi nchi maskini ni kujidanganya kuwa umaarufu na utajiri utafika kwa kukaa kijiweni na kubabaisha. Lugha dhaifu mathalani Kiingereza cha Kimarekani chenye maneno machache ya matusi tuliyoyasikia katika nyimbo za Rapu ama sinema za wamachinga, zinatumika. Kujidanganya kwetu kunazusha tabia ya kutofanya kazi,kutoongea lugha inayoeleweka; kutosoma vitabu, kifupi; ulimbukeni.
Na moja ya tatizo ni kuinua vyuma kwa pupa.
Kama tulivyoona makala zilizopita mazoezi ya uinuaji vyuma yanaenea kasi sana duniani. Huku Majuu wanaume kwa wanawake wanachapa vyuma. Wanawake wanainua kusaidia miili inyooke na kupendeza zaidi; wanaume kujenga musuli na nguvu. Wanaume Tanzania tunainua vyuma bila kujua namna.
Karibuni nilikuwa na kijana aliyefika London kikazi. Tulipokwenda Gym nilimshangaa ; mara ainue hiki mara kile ili mradi anataka musuli haraka haraka.
Utafiti uliofanywa Sweden na kuchapwa gazeti la afya mwezi huu (Men’s Health) limesisitiza kwamba mwanadamu ukifanya mazoezi ukiwa kijana umri wa 20 hadi 40;ni rahisi kwako kukwepa maradhi ya moyo ukizeeka zaidi. Ndiyo maana wanamichezo huishi maisha marefu; ila wanaofariki mapema ni baadhi ya wanariadha waliojenga tabia za kuvuta sigara, ulevi au kupatwa na ajali zisizozuilika. Aghalabu basi, takwimu za kisayansi zinathibisha maisha marefu unapofanya mazoezi.
Kwetu Bongo kuna watu wa aina mbili; wenye uwezo wa kufanya mazoezi na kupenda kuyafanya, na wasioweza kuyafanya ama kwa kuwa hawaoni haja yake, hawataki au hawajiwezi.
Tuwaangalie wa kwanza.
Kama una uwezo wa kufanya mazoezi ya kuinua vyuma unatakiwa uwe na ratiba nzuri. Ujue kwamba unafanya siku kadhaa na kupumzika siku kadhaa. Wataalamu wanasisitiza siku usizofanya mazoezi ndizo mwili hujijenga; na lazima kunywa maji na kula vyema siku hizo. Jambo la pili, hakikisha unajua lengo ni nini. Je, ni kujenga viungo vipi? Je, unapotumia vyuma unaviinua kuendeleza nguvu za kimichezo (kama ubondia au mbio) au kupunguza unene? Watalaamu wanasisitiza kuweka muda wa mazoezi kati ya dakika 45 hadi 60. Ukizidisha sana muda unachokesha viungo na kusababisha maradhi siku za uzeeni. Lazima uanze mazoezi kwa kuuchemsha mwili, ama kwa mbio fupi , kutembea haraka au mashine za kukimbiza moyo na damu (treadmill). Ukishahema sasa jinyooshe halafu anza na sehemu fulani za mwili (labda tumbo au mikono).
Unatakiwa uhesabu kila unachokifanya. Kama unafanya mazoezi ya tumbo hesabu mara unazoweza; pumzika dakika chache, kisha rudia mara mbili au tatu. Ukishamaliza nenda kiungo kingine. Mbongo niliyemsema juu alinidokeza vijana wengi nyumbani hawajui wanatakiwa kufanya mahesabu.
Ukimaliza tuliza mwili kwa mazoezi mepesi ya kujinyoosha au tembea. Hakikisha unakunywa maji kidogo kidogo wakati ukifanya mazoezi, na ikiwezekana ule tunda kama ndizi mbivu mara tu ukishamaliza. Ulaji unatakiwa uwe wa mpango. Usile hadi tumbo likajaa sana; ila kula milo midogo midogo ya mara kwa mara.
Kwa wale wanaotaka kupunguza vitambi; tukumbushane kwamba matumbo makubwa hayawezi kupungua kwa mazoezi ya tumbo ( “sit ups”) peke yake. Kuvimba tumbo hutokana na kula sana vyakula vya mafuta na wanga bila kufanya mazoezi. Hivyo kuviondoa kunawezekana tu kwa kupunguza kula sana huku ukifanya mazoezi yanayotoa jasho (Cardio).
Kama unapenda kula chakula kingi; gawa ulaji wako uwe mdogo lakini wa mara nyingi. Wataalamu wanasisitiza kuwa kila mtu anatakiwa ale mlo unaolingana na ngumi zake mbili, umbo la tumbo lako. Kiasi hicho tu ndicho kinachotakiwa mwilini. Mlo kuzidi ngumi mbili zako hugeuzwa kinyesi au mafuta.
Kwa wasiokuwa na muda wa mazoezi; niwape ushauri mmoja. Tafuta dakika kumi hadi ishirini kila baada ya siku chache kufikiria namna ya kujiboresha.
Juma lililopita tuliona namna kila kipindi cha miaka Hamsini iliyopita kimekumbwa na mambo yaliyotufanya wanadamu tuone mwisho wa dunia ni huu. Lakini hayakuanzia mwaka 1962.
Miaka ya Hamsini kulikuwa na ukoloni Afrika nzima kwa hiyo hasira na chuki zilienea; miaka ya Arobaini vita vikuu vya pili vya dunia vinakisiwa kuua watu kati ya milioni 50 hadi 70; mara mbili ya idadi ya Watanzania! Miaka ya 1930 ilikuwa na matatizo makubwa ya uchumi yaliyowatesa mababu na bibi zetu. Kabla ya hapo vilikuwa vita vikuu vya kwanza vilivyoua milioni 16. Karne ya 19 ilijazana vita na mizozo ya kikabila na ujio wa ukoloni kuanzia 1884 hadi vita vya Maji Maji vilivyomalizika 1907. Wakati huo watemi na wamangi wetu walinyongwa na kudhalilishwa na Wajerumani. Kifupi hatujawahi kuishi nyakati nyeupe bila madoa. Hii ndiyo kauli na harakati za uhai.

-London, Jumatatu, 3 Januari, 2011
Ilitoka gazeti la Mwananchi Jumapili tarehe 9 Januari:
http://mwananchi.co.tz/mwananchi-jumapili/38-johari/8187-kujiendeleza-mazoezi-kuinua-vyuma-2

No comments:

Post a Comment