Monday 17 January 2011

MECHI YA ARSENAL UWANJA WA EMIRATES LONDON...

Niko uwanja wa Emirates, kaskazini ya London.
Ili kuingia hapa yabidi tukae foleni ndefu iliyoanzia milango mikubwa inayolindwa na askari doria juu ya farasi. Ingawa baridi ya leo kali wale askari wamesimama macho makali wakituangalia kama siafu tayari kung’ata. Si Arusha, si London; askari ni askari.
Emirates iko kitongoji cha Islington. Miaka yote niliyoishi mjini London huzijua mechi za Arsenal  maana si mbali  na ninapoishi; jirani na Tottenham Spurs maadui mwitu wa Arsenal. <!--more-->
Huu ni msimu wa barafu linalodondoka kama mvua ya manyunyu. Kila mmoja wetu kavalia makoti mazito, fulana mikono mirefu, kofia zilizofunika vichwa, masikio  na leso nzito za kukinga shingo na vifua. Mikono imefunikwa kwa maglavu ya sufu na baadhi ya ajuza waliokuja mpirani wamebeba mikongojo wasiteleze. Kila tunapokanyaga  kelele za Kocho! Kocho! Kocho! juu ya kokoto la barafu zinasikika maana tumevalia mabuti makubwa ya msimu huu wa kutisha Ulaya.
Mara nakumbushwa zamani nikikulia mgombani Moshi na Arusha  miezi ya masika. Mbali na matope na utelezi, zilipita nyungunyungu na konokono. Mvua za nyanda za juu Afrika hutaabisha magari na wakazi wake; ila maisha hayasimami. Ndivyo pia Uzunguni; ingawa barafu ni ukiwa mtupu, binadamu hawaachi kwenda kazini wala stareheni.
Si ajabu basi hapa Emirates, wapo pia watoto, mama na baba zao ; hata mababu wakipambana na ubaridi mkali unaojaribu kila njia kupenyeza mavazi tuliyojigubika.
Ingawa foleni ni ndefu, utaratibu wa Kizungu ni kupeleka mambo haraka. Huwezi kuja hapa bila tiketi, kwa hiyo mpango uliopo ni kuonyesha tu nakala uliyoshanunua mtandaoni ikakatwa nusu, kisha ukaelekezwa kwa askari wanaokagua. Nje haparuhusiwi kabisa wauza tiketi za magendo au wamachinga; macho ya askari na kamera za video zinachunguza kila kitu...
Ukishapita foleni huruhusiwi kuingia na chupa, kinywaji au kisu. Ukishapekuliwa unapita na kujikuta ndani ya vyumba vikubwa vya kuingilia uwanjani. Vyumba hivi vina mabaa na mijigahawa inayouza vitafunio, vinywaji, bendera na skafu za rangi nyekundu na nyeupe; rangi rasmi za timu ya Arsenal. Ukitaka kuingia na bia unalazimishwa uimimine ndani ya bilauri za plastiki. Hii ni kwa usalama; zamani watazamaji walikuwa na tabia ya kuwatupia wachezaji vyupa.
Ewalla.
 Ninapoingia vyoo vya Emirates nakumbuka mwaka 1988 nilipotazama mechi ya Brazil na Argentina uwanja wa Maracana mjini Rio De Janeiro. Alicheza pia mwanasoka maarufu, Diego Maradona. Kwa kuwa Brazil na Argentina ni kama paka na mbwa; ilikuwa vigumu kwangu na wenzangu  kumshangilia Maradona. Kila alipogusa mpira, Wabrazili walimzomea. Sisi wachache tulimshangilia  alivyosakata chenga za kipekee. Wakati wa mapumziko tuko chooni; likaja kundi la Wabrazili.
“Nyinyi mnashangilia Argentina?” Akauliza mmoja, kwa Kireno.
“Hapana, tunamshangilia Maradona,” Mmoja wetu akajibu.
Mwingine akaongeza. “Anacheza kama Pele!”
“Mtusamehe hatujawahi kumwona mchezaji mahiri hivi,” Nikafafanua kiangalifu.
Pale msalani pakawa kama pamedondoka bonge la joka.
“Sikilizeni! Mkitaka kutoka hapa salama leo basi muache upumbavu wa kuwasifia hawa washenzi !”
Kilikuwa kitisho bab kubwa. Hadi leo nikiwa vyoo vya viwanja vya mpira nakikumbuka.  Ila hapa Emirates mambo tofauti; washabiki wa Arsenal wako vyoo vya upande mmoja na wa upinzani mwingine; hakuna maadui kukutana.
Tumo, tumo...
Emirates iliyofunguliwa rasmi mwaka 2006, ina nafasi ya watazamaji 60, 355 ambapo Old Tafford wa Manchester United ni 75,957.
Timu ya Arsenal ilianzishwa mwaka 1886 kitongoji cha Woolwich Arsenal ambapo siku hizi pamebakia tu jela maarufu ya Belmarsh. Mwaka 1913 ilihamishiwa kaskazini baada ya wafanyabiashara kugundua sehemu hiyo haikuvutia wateja. Arsenal ni timu pekee iliyowahi kucheza misimu miwili mfulululizo bila kufungwa na klabu yeyote, mwaka 2003 na 2004. Kitendo hicho kilichowakatia jina la “Invicibles” kimewahi kuonyeshwa na timu moja tu katika historia ya ligi ya Uingereza; yaani Preston mwaka 1888 - 1889.
Uwanja unanguruma.
Nipo karibu na walipokaa ustaadh Arsene Wenger na makocha wapinzani wa Wigan.
Jambo muhimu unalogundua ukikutana na watu mashuhuri ni jinsi walivyo tofauti na vile tunavyowadhania. Nilipokuwa Bongo nilijiuliza kwanini wachezaji wetu wa kitaifa wadogo vile kiumbo?
Lakini ninapokaa hapa nikiwaangalia Samir Nasri, Theo Walcott,  Cesc Fabregas na hata kocha mwenyewe, Wenger, nashangaa walivyokuwa pia wadogo wa umbo.
Mpira umeanza.
Watazamaji wanaimba:
“Red Army! Red Army!” (Jeshi Jekundu); huku Wigan ikijaribu kila njia kuzuia kipigo. Natetemeka kwa baridi; uwanjani barafu linaanguka. Namwangalia golikipa wa Arsenal (mwenye jina gumu), Wojciech Sczcesny, akiruka ruka ajipe joto. Hana kazi kubwa leo maana washambuliaji wa Wigan hawajapata mwanya. Ghafla Eboue kachomoka; kampa pasi Fabregas; Fabregas katoa ukanda kwa Theo Walcott anayekimbia kijogoo. Mpira wa kupendeza; lakini Walcott kategewa kaanguka.
Uwanja mzima : Aaaaaah!
 Baada ya dakika kumi na tano bila bao lolote kufungwa watazamaji wanaanza kuimba kwa nguvu:
“You dirty northern northerners!” (Nyinyi wapumbavu toka kaskazini), maana Wigan kwao kaskazini ya Uingereza.  Mpira unaendelea hadi mapumziko bila bao lolote. Wakati wachezaji wakienda kupumzika, wimbo maarufu dhidi ya maadui wa jadi unarindima:
“Stand Up If You Hate Tottenham!” (Simama kama unaichukia Tottenham)! Kila mtu anasimama.
Ila kinalonishangaza ni namna starehe ya mpira ilivyobadilika. Miaka ishirini iliyopita niliwahi kutazama mechi ya Liverpool. Nakumbuka namna wanaume walivyolewa wakitafuta ugomvi.
Leo Emirates wamejazana wanawake, watoto, wazee; kifupi, familia. Wapo vigoli waliokuja peke yao kama Joanna, Mmarekani anayepiga picha.
“Vipi ? Unafurahia mechi?” Namuuliza.
“Sana. Mi lakini mshabiki wa timu ya wanawake wa Arsenal. Nampenda sana Kelly Smith.”
Timu ya wanawake ya Arsenal ni klabu bingwa kushinda zote Uingereza. Iliundwa mwaka 1987 na imeshatwaa vikombe 33 vikiwemo ligi za kitaifa za wanawake na Ulaya (UEFA). Kutokana na ufundi wake Kelly Smith ambaye (mshambuliaji) ni mchezaji wa timu ya taifa ya wanawake Uingereza, kaitwa Zinedine Zedane wa kike.
Mapumziko yamekwisha.
Mechi inaendelea na  mwisho Arsenal wanashinda kwa mabao mawili. Wakati tukipambana na “tope” lile la barafu watazamaji waliohamasika wanaimba wimbo :
“Who are you? Who are you?” (Nani wewe)
Natetemeka baridi nikikimbia na wenzangu. Najiuliza vipi wale wachezaji walimudu kucheza dakika tisini ndani ya barafu? Ama kweli kila mtu na ajira yake.

 -London, Jumanne, 11 Januari,  2011

Ilitoka Mwananchi, Jumapili 16 Januari, 2011.

http://www.mwananchi.co.tz/mwananchi-jumapili/38-johari/8405-nipo-ndani-emirates-wa-arsenal

No comments:

Post a Comment