Wednesday 11 May 2011

MTANDAO WA VIJANA TANZANIA : MAHOJIANO NA MICKEY “MIKIDADI” JONES MKAZI DENMARK NA LYDIA MKUDE ANAYESOMA, UGANDA...

Hali ngumu ya uchumi na maendeleo imezusha vijana wengi wasio na kazi; wanaranda randa ovyo barabarani, wakitega  na kusogoa vijiweni, wakijaribu hili na lile. Watoto yatima hawana wazazi kutokana na maafa ya maradhi ya Ukimwi na jamii yetu inazidi kukuuza wananchi wasiokuwa na matumaini. Yote haya yanaweza kumea hasira, kero na ghasia tupu.
Miezi michache Mickey Mikidadi Jones alikuwa likizo nyumbani. Hali ilimkuna sana.
Leo Mickey Mikidadi  Jones,  kaamua kujihusisha  na mtandao wa kuwaunganisha vijana  wa ughaibuni na kwetu Bongo kuboresha maisha yao. Mara nyingi nilipomhoji Mickey alimtupia maswali dada Lydia Mkude, ambaye ni mshauri mkuu wa MMVT ("Mtandao wa Maendeleo ya Vijana Tanzania").


Solomon Gaddi (mwenyekiti wa MMVT) akihutubia kikao. Kushoto kwake ni Haruna Mbeya (mwakilishi , Ughaibuni) na mwanzo kabisa Mshauri na mwakilishi wao wa kimataifa mtandaoni, Mickey Mikidadi Jones.   Picha ihsani ya MMVT.

 <--more--!>

 Nafasi yake Mickey Mikidadi Jones si kuwa "kiongozi" bali  kiungo  na mshauri mkuu wa mtandao huu kufuatana na uzoefu wa mfumo wa maendeleo ya vijana katika nchi zilizoendelea ughaibuni. Chini anashirikiana bega kwa bega na dada Lydia kujibu maswali.
Swali:  Mickey mtandao wa MMVT utasaidiaje Watanzania?
Mickey Jones: Utawasaidia Watanzania wenzangu katika nyanja tofauti za kimaisha kijamii, kiuchumi pia kisiasa ili kwa pamoja tuweze kujikomboa na hali ya kimaisha katika kujenga taifa letu kupitia vijana.
Swali: Je una nini cha kuwaeleza Wabongo wanaoishi Ughaibuni? Je watawezaje kusaidia nyumbani hasa ikiwa wengi wana kipato kizuri na wanaharakatika pia  na maisha yao?
Mickey Jones: Mimi nawashauri tusikate tamaa  kutafuta maisha ya sasa na baadaye kwa sababu katika maisha hamna jambo lisilowezekana chini ya jua, ulimwenguni. Pia nawaambia tusisahau nyumbani kwa sababu “nyumbani ni nyumbani” hata kama unalala nje. Kwa kufanya hivyo tujenge taifa letu kwa ujumla.
Swali: Ulinieleza uliporudi awali kwamba kielimu vijana wa Kibongo wamedidimia kuliko enzi za Mwalimu Nyerere. Je nini hasa wasichojua? Mbona shule ni nyingi zaidi ya enzi za Ujamaa?
Mickey Jones: Wengi wa vijana wa Kitanzania wanatakiwa mashuleni wapatiwe pia elimu ya kijamii ili wajitambue kwanza. Si kwamba hawajui bali wanatakiwa kupata mwongozo wa hali ya juu pia marekebisho katika mtaala mzima wa elimu ili elimu yetu izidi kuwa juu zaidi. Kuwa na majengo mengi ya shule na vyuo si hoja. Unaweza ukawa na pesa na akili nyingi na usijue matumizi yake...
Swali: Je, Bongo pana amani na ahueni miaka ya mbeleni?
Mickey Jones: Watanzania tunatakiwa kuilinda amani ya nchi yetu kwa sababu bila ya kufanya hivi tutaelekea pabaya. Tukae chini kwa pamoja tutafakari tufanye nini ili kuijenga nchi yetu katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo ; sio kutafakari kuvuruga amani, upendo, ulinzi wa nchi yetu kwa miaka ya mbeleni na hata sasa.
Swali: Nini cha zaidi utawaeleza vijana wetu?
Mickey Jones: Kwa pamoja Tanzania tujenge na kuilinda amani ya nchi yetu kupitia hawa vijana wetu wa sasa. Wao ndiyo wanaostahili hasa kulijenga taifa  la sasa kupitia mwongozo na ushauri mbalimbali kutoka kwa waliotangulia (yaani wakubwa zao). Vijana wanaweza kuwasiliana nami kwa simu + 45 – 50192471
Au pia barua pepe:mickeyjohnamos@yahoo.com
Kufafanua zaidi mtazamo wa Mtandao wa Maendeleo ya Vijana Tanzania; niliongea vile vile na Lydia Mkude anayesoma Kampala International College.
Swali: Je mtandao ulianzishwaje?
Lydia Mkude: Kama vijana tulikutana katika mambo ya kielimu tulikaa chini na tukafikiria kuanzisha chombo kitakachowapa vijana sauti moja katika nyanja mbalimbali za kimaisha kijamii, uchumi na kisiasa.
Swali: Mtandao wa MMVT utawasaidiaje vijana ndani na nje ya nchi?
Lydia Mkude: MMVT itawasaidia vijana kupitia idara zilizopo kujipatia nafasi mbalimbali za mawasiliano baada ya kukaa miaka mingi bila kujishughulisha; utawasaidia pia kupitia misaada na vianzisho mbalimbali kutoka wafadhili na watu mbalimbali. Misaada pia itatoka kupitia elimu. Maana katika mtandao huu kuna idara mbalimbali za afya, elimu,mawasiliano na utafiti, mazingira na uchumi.
Lydia akihutubia kikao...picha ihsani ya MMVT


Swali: Nini zaidi?
Lydia Mkude : Kutakuwa mikutano na semina mbalimbali ambazo vijana watakuwa wanazipata kupitia mtandao...Ukitaka habari zaidi wasiliana nami: lydiathadeous@ymail.com au Simu: +256-787928020
Swali : Je kuna mradi wowote kilingeni au jambo lolote mnalolifanya sasa hivi ambalo laweza kuvutia macho na masikio?
Lydia Mkude: Kwa sasa hakuna mradi wowote; vijana wanajitolea kuchanga na kutoa ala mbalimbali katika shughuli za mtandao...
Swali: Je Rais Kikwete anaufahamu mtandao?
Lydia Mkude: Kwa upande wetu tuna matumaini anaujua...
Swali : Je kwa sasa ni wanawake wangapi wanahusika na mtandao?
Lydia Mkude: Kwa sasa idadi ya wanawake ni kama asilimia 40 (takribani sawa na wanaume) vile vile tunatia nguvu ili wazidi kujiunga na mtandao...
Swali: Je vijana wanaotaka kujiunga nanyi watawasiliana vipi na MMTV?
Lydia Mkude: Kupitia mitandao yetu kama Twitter, Yahoo, Facebook , Simu, kuhudhuria mikutano na semina mbalimbali zinazofanywa na vijana kila wiki, mwisho wa mwezi na mwaka...

-Makala ilitoka pia safu ya "Kalamu toka London" gazeti la Mwananchi, Jumapili 8 Mei, 2011.


No comments:

Post a Comment