Monday 25 July 2011

BLOG LA “MWANAMKE NA NYUMBA” MFANO WA UANDISHI UNAOANGALIA MAHUSIANO NYETI YA MTANZANIA...

Uandishi wa mablogu wahitaji tarakilishi. Tarakilishi ni neno fasaha la Kiswahili linaloimanisha Kompyuta. Na hiki si chombo tu cha kuandikia. Huendesha simu za mkononi; taa zinazoongoza magari barabarani, mitambo ya ndege, mahospitali, runinga, nk. Dunia ya leo inaongozwa na tarakilishi. Hili ni bado somo jipya Tanzania. Kidunia mtandao kama tunavyoujua una miaka 15 ingawa sayansi hii ya kihabari imekuwepo kwa takribani miaka 30. Awali ilitumiwa na watu wachache hasa wanajeshi na majasusi kulinda matakwa ya serikali mbalimbali.
Rosemary Mizizi, blog lake Mwanamke na Nyumba linazungumzia mahusiano nyeti kati ya wanawake na wanaume  kwa undani sana katika jamii ya Tanzania leo.
<--more--!>

Leo ni asilia ndogo sana ya Watanzania wanaotumia tarakilishi; mosi ni aghali na pili, umeme ni kitengo kichanga na cha matatizo Afrika Mashariki. Bado ni rahisi kusoma magazeti na kuwasiliana kwa simu ya mkononi kuliko kutumia mitandao.
Kwa nchi zilizoendelea mawasiliano ya mtandao yameletwa majumbani. Ukinunua “laptop” ya bei nafuu (kama shilingi laki nne) unamudu kutumia pia runinga, simu ya ndani, mtandao (unaoitwa Broadband) ili mradi ulipe ushuru mdogo kila mwezi. Lengo la serikali na makampuni makubwa ni kurahisisha mawasiliano haya kutangaza habari na kumuuzia kila mwananchi bidhaa.
Uzuri wa mtandao ni huo.
Ukiweka picha ya video katika uwanja wa You Tube, mathalan, ni rahisi kuitangaza kupitia nyenzo nyingine kama Facebook (uwanja wa marafiki duniani), Twitter (mawasiliano mafupi ya haraka) na kadhalika. Ukimwandikia mtu barua pepe ni unaweza pia kutangaza anuani ya tovuti la shughuli zako.
Uandishi wa mablogi ni kati ya mapinduzi makubwa yaliyofanywa mtandaoni. Blogi ilianza kama muhtasari wa habari ya mtu mmoja miaka 15 iliyopita. Badala ya kuandika mambo yako ndani ya kitabu ukayaficha kabatini; unayatangaza hadharani. Leo blogi zimekuwa sehemu mahsusi ya mawasiliano. Vyombo vya habari na runinga zina blogi. Watu mashuhuri, wafanyabiashara, wanamichezo na hata viongozi wa kisiasa wana blogu. Aidha blogu hazifaulu kama wewe mbinafsi au mchoyo. Ukirusha jambo unaruhusu pia wengine kuandika mawazo kukusifia au kukinzana nawe.
Mbali na kublog na kupiga picha Jestina George ni msanifu wa mavazi kama anavyoonekana katika maonyesho ya Anna Luks (mwana mavazi wa Kitanzania) mjini London majuma mawili yaliyopita...
Tovuti la “Zoom Tanzania”  linalotangaza habari mbalimbali za Bongo (hasa utalii) karibuni limeorodhesha blogu kadhaa zinazosomwa zaidi nchini mfano ile ya Issa Michuzi aliyeanza shughuli hiyo miaka sita iliyopita.
 Subi Nukta  ana spidi kali kutokana na wepesi wake kuchangia hoja mitandaoni. Jina lake liko kila mahali.  Huandika usiku na mchana kupitia mitandao mbalimbali ya redio, Twitter na Facebook; akichanganya habari, misemo na majadiliano ya haraka haraka...
Kifikra dunia ya leo imetawaliwa na waandishi wa kiume. Masuala ya mahusiano hususan mapenzi  kupitia riwaya za Kiswahili  yameandikwa ama kutungwa na wanaume. Magwiji maarufu wa Kiswahili ni wanaume: Shaaban Robert (enzi za ukoloni), Faraji Katalambula (miaka ya 60 na 70)  Mohammed S. Mohammed ( kitabu mashuhuri cha mapenzi “Kiu” mwaka 1970), Said Ahmed (Asali Chungu na vitabu mbalimbali ) anaendelea kuandika pia miaka hii kama akina: Adam Shafi (Vuta Nkuvute), Elvis Musiba, Ben Mtobwa, Eric Shigongo  anayemiliki mtandao wa Global Publishers, Juma Kidogo, nk. Ukifukua zaidi vumbi na mchanga wa fasihi ya Kiswahili utagundua ingawa wasomaji wengi nchini ni wanawake; ni wachache sana wanaoandika.
Ila ukiendelea kutimua vumbi utawakuta wanawake wachache wakijitahidi kuandika mablogi.
Jacquiline Kibacha aliyeshinda tuzo la Ushairi Uingereza, (Beffta, mwaka 2009) amekuwa aki blog miaka mingi na hutumia jina la "Pretty Poet"...
Utamwona Shama Jaffer (Candle Heart); Jacquiline Kibacha Jacquiline Kibacha wanaoandika Kiingereza; Jestina George anayechanganya Kiingereza na Kiswahili anayedonoa mseto wa mavazi, urembo na habari; Subi Nukta anayetathmini habari; Miriam Love anayekuuza mapishi ya Kitanzania ughaibuni na Yasinta Nyongani anayeandika Kingoni na Kiswahili.

Yasinta Nyongani...mwenye mtindo wa kipekee kabisa unaochanganya uzalendo, fasihi, uke, mila na mapenzi ya Uafrika...

Hata hivyo kitakwimu waandishi hawa si wengi ukilinganisha wanaume.
Halafu yupo Rosemary Mizizi.
“Mke Na Nyumba” si miongoni ya mablogi yanayosemwa semwa sana Bongo. Pengine kwa vile halizungumzii masuala mazito ya kinchi na kisiasa. Si kwamba masuala ya kisiasa si muhimu. La hasha. Ila kuandika mambo yanayotendeka ndani ya nyumba zetu, baada ya milango na madirisha kufungwa si suala jepesi. Rosemary Mzizi kawa muwazi anapotangaza kuwa ataangalia ndoa na kusisitiza kuwa “ mume, mke, mpenzi, watoto” wanapotaka ushauri wakutane ndani ya blogi lake. Kinyume na mablogi mengine yanayotangaza habari na kuleta mapya hili limechagua mada moja na kuikalia.
Maudhui yake yahusu undani wa desturi zake mfano ile inayoongelea umuhimu wa mkeka. Kwamba mkeka unaweza kutumika kulia chakula au faraghani chumba cha kulala. Kwamba mkeka si tu jadi ya watu wa pwani.  Anakuuza utamaduni wa vifaa vya ndani na kukumbusha mila na desturi. Mkeka anasisitiza ni moja ya “zawadi kuu za ndoa” hivyo matumizi yake mengi.
Suala nyeti la magovi na tohara za wanaume ni kati ya mambo mazito yanayoangaliwa bila wasiwasi katika blog la Mwanamke na Nyumba. Hoja na maoni kusisitiza usafi na ubora wa tohara hii umeangaliwa kwa undani.  Karibuni,  Umoja wa Mataifa umesisitiza haja ya kuondoa magovi kama moja ya kinga dhidi ya  UKIMWI...

Naam!
 Anapakua visa vya wafanyakazi wa ndani na waajiri wao kimapenzi; suala ambalo Wabongo wanalifahamu(ningependa pia aangalie unyanyasaji wa wafanyakazi hawa lakini lengo lake ni kuchambua ngono kati ya waajiri na waajiriwa). Anatazama tatizo la urijali na ukosefu wa nguvu za mapenzi kwa wanaume. Anaangalia  suala la “Vyoo vya Nje” kwa maskini wasiomudu kujisaidia ndani wakatoka huku wamejifunga kanga au taulo.  Kawahoji wanawake mbalimbali kuhusu nini hasa wanachokipenda katika mwanaume. Wahojiwa wanasema ukweli usiosikika katika fasihi za wanawake wa nchi maskini. Hapa ndipo ulipo umuhimu wa maandishi ya kike.  Moja ya faida zake ni kujua nini hasa wanawake wanachotaka. Je kwa nini wanaume wengi wanashindwa mahusiano? Je, mwanamke anaridhika na pesa na utajiri tu wa mwanamume? Nini kinachoharibu au kuvunja ndoa zetu? Kwanini wanaume na wanawake pia hulala nje ya ndoa? Je, kwanini ngono na mapenzi ni suala muhimu sana katika ndoa? Je, ubinafsi wa wanaume au wanawake unachangia vipi katika kutoridhishana?  Je watoto wanarudhikaje kutokana na wazazi wa kambo? Je watoto hao hao wanawezaje kumdhuru mama wa kambo?
Blogi hili limejaribu sana kugusa suala nyeti la mahusiano katika jamii yetu. Ila kinachokera katika uandishi wa blogi nyingi zinazoandikwa na vijana wa leo Tanzania ni suala la matumizi ya Kiswahili. Mwandishi Rosemary Mizizi hatumii lugha chachu yenye maneno ya Kiswahili na Kiingereza (kama wanavyotumia baadhi ya waandishi wengi chipukizi). Kosa lake dogo ni moja. Kutoandika maneno sawasawa. Huandika “wanadhamini” badala ya “wanathamini”; “Kufatwa” badala ya “kufuatwa”; “umri umeenda “ kinyume cha “umekwenda”...”Mkaka” (kaka) “Mdada” (dada) ; “Masifa”(sifa) nk.
Mifano hii inadhihirisha ilivyo haja ya waandishi wetu kuboresha lugha zao. Wananchi hufaidi kuwasoma kimaudhui na hapo hapo tunajifunza. Yumkini yatubidi waandishi tuwe macho kuimarisha matumizi ya sarufi, misamiati, nahau, nk. Waandishi ni viongozi wa maendeleo ya lugha katika jamii.  Kama inavyothibitishwa na Rosemary Mizizi, waandishi stadi wa Kiswahili wapo; tena wanajitahidi. Wajibu na nafasi yao nzito.  

Ilitoka Mwananchi Jumapili Julai 17, 2011.
http://www.mwananchi.co.tz/editorial-analysis/47-kolamu/13509-kutoka-londonblogu-za-wanawake-ni-chachu-ya-uhusiano-katika-jamii.html

No comments:

Post a Comment