Sunday 28 August 2011

KIFO CHA MWANAMUZIKI AMY WINEHOUSE NA FUNDISHO KWETU BONGO

Moja ya nyumba zilizoporwa wakati wa ghasia mjini London majuma mawili yaliyopita ni ya  mwanamuziki maarufu wa Kiingereza , Amy Winehouse aliyefariki mwezi Julai.
Ingawa uchunguzi wa nini hasa kilichomuua ungali ukiendelea hadi Oktoba, Amy Winehouse alifahamika kuwa mchapa pombe kali na dawa za kulevya wakati wa maisha yake mafupi ya miaka 27.
Mwanamuziki huyu Myahudi alikuja juu 2003 kutokana na kipaji chake cha sauti nzito ya kupendeza juu ya utenzi wa maneno  aliyoyaandika kwa ustadi sana.
Akiwa shuleni alifukuzwa sababu ya tabia ya bashasha, kutosikiliza aliloambiwa, kutoboa pua. Aliimba kila mara darasani akawakera waalimu. Ingawa hakuwa bado mlevi ufundi  wake wa muziki (alipiga pia gitaa) ulimpatia nafasi ndani ya vyuo mbalimbali vya sanaa ikiwepo Sylvia Young Theatre School.


Amy akiwa na babake Mitch Winehouse. Picha  Shaun Curry wa Getty Images.
<--more--!>
Kawaida vijana wanaokulia jiji hili huathiriwa na tamaduni za wakazi wa hapa. Kitwakimu lugha 300 zinazungumziwa London. Kati ya desturi za mavazi, muziki na lugha zinazowagusa vijana ni za watu weusi  toka visiwa vya Karibi (Jamaika, Trinidad, Guyana, Barbados nk)  Marekani na Afrika.  Si ajabu basi muziki wake Amy Winehouse ingawa Myahudi (mama Mrusi) unanuizwa na Jazz, Reggae na Soul. Sauti yake nzito ilifananishwa na waimbaji magwiji weusi wa kike akina Nina Simone, Aretha Franklin, Sarah Vaughan.
Sarah Vaughan, mahiri, jalalati na jamila; mwimbaji mwenye sauti nzito ya Jazz. Alifariki mwaka 1990...

Babake marehemu, Mitch Winehouse, (miaka 60) ambaye ni dereva teksi, alikuwa karibu sana na binti hasa kutokana na alikuwa pia mwimbaji wa Jazz. Miezi michache kabla ya janga, shughuli  yake ya kuimba Jazz (ambayo haikuwahi kuonekana) ilipata msukumo mpya kutokana na mafanikio ya binti. Wakati Amy akifariki baba mtu alikuwa safarini New York akiimba Jazz yenye mizizi ya Wamarekani weusi.
Wengi wa wanamuziki katika bendi yake Amy walikuwa weusi. Meneja  na hata mlinzi aliyeifumania maiti yake mchana ule wa Jumamosi tarehe 23 Julai, kitongoji cha Camden Town alikuwa pandikizi la njemba asili ya Kiafrika.
Wapenzi wake Amy Winehouse walakin, walikuwa Wazungu. Mume wake walioshaachana na  ambaye hadi leo yuko jela, Blake Fielder Civil ndiye aliyemdumbukiza choo cha unga wa Cocaine na Heroin. Unapokuwa mlevi wa Heroin yakubidi ujidunge sindano. Mashimo ya sindano yanapouzidia hukubidi utafute sehemu  muafaka mwilini na hiyo ni karaa tupu. Karaa hii inaanza kunawiri Bongo na Visiwani. Vijana wanaochangamkia Heroin wanasahau kwamba kwa maskini kujitwisha asali hii chungu ni  safari ya kifo. Mbali na wazimu wa kuisaka pesa kwa namna yeyote kusudi upate “nishai” Heroin ni kati mwambukizaji mkuu wa UKIMWI kutokana na kushirika wa vijisindano. Kwa maskini Afrika ni kama mtu gizani kuvaa kaniki kisha akajipaka masizi eti wanja.
Basi haikuwa ajabu Amy Winehouse kuonekana siku nyingine anavuja damu miguuni kutokana na uboza huu.  Yeye na mumewe Blake walipigwa picha magazeti ya umbea, miguu mitupu usiku wamelewa na kuvimbiana baada ya kuchapana masumbwi.  Walipoachana baada ya Blake Fielder kufungwa jela Amy alisisikita sana akaendelea kumtungia nyimbo za mahaba. Albam yake ya pili “Back to Black” iliyotolewa 2006 ikashinda tuzo nyingi ikiwemo “Grammy” ilitota dhamira ya mapenzi kwake mtemi wake huyo aliyeko bado jela leo Jumapili.  
Kisa cha mapenzi ya wasichana maarufu waliotoka familia nzuri kisha wakakutana na washashi waliowaharibia ndilo fundisho letu la pili. Mfano mzuri ni mwimbaji maarufu wa miaka ya Themanini, Whitney Houston. Whitney alilelewa mazingira ya dini, heshima na staha.  Alikuwa na undugu na mwimbaji maarufu Dionne Warwick. Mama Warwick anasifika kwa kibao kitamu alichotoa mwaka 1964 “Walk On By”…
Akiwa bado mbichi, Whitney Houston aliwika kijogoo 1985 na albam “How Will I Know” (Nitajuaje).  Sauti yake kali, ya juu, safi, maridadi, ilianza kuharibika alipokutana akaolewa na Bobby Brown. Licha ya dawa za kulevya Brown alimkandika  magumi  Whitney Houston. Miaka michache iliyopita Whitney alizomewa katika maonyesho yake hapa Uingereza.  Haiba yake ya mwanamke mweusi mwenye ngozi nyororo na matao ya kuvutia imebabuka, hafahamiki tena. Mwezi Machi, Bobbi Kristina, binti yake wa miaka 18 alipigwa picha akigumumia unga wa Cocaine. Mtoto Umleavyo Ndivyo Akuavyo.
Mbali na afya tabia hii humaliza pesa. Yasemekana mama Bobbi humpa msichana Dola elfu moja (shilingi moja na nusu) kwa juma ambazo huishia katika nishai.
Amy Winehouse vile vile.
Aliharibu maonyesho kutokana na usaha huu; akaacha nyimbo katikati, alikosea maneno akashindwa kabisa kuhudhuria shoo alizolipwa maelfu ya fedha.  Onyesho lake la mwisho mjini Belgrade lilisimamishwa. Alitetesuka jukwaani , akibwabwaja ovyo na video iliyoko You Tube inamwonyesha akizomewa kisha akimrushia mtazamaji chombo cha kuimbia (maikrofoni).
Amy Winehouse keshazikwa.
 Wasanii wengi matajiri na maarufu wanadekezwa. Mwana mitindo Kate Moss kapigwa picha mara kadhaa akinusa unga na hata hivyo anaendelea kuuza na kuuzwa. Mwanamuziki Pete Doherty aliyekuwa bwanake Kate Moss keshapelekwa mahakamani mara 13 kutokana na dawa za kulevya, fujo, mauaji, nk.

Mwanamuziki na mtunzi wa mashairi Pete Doherty na mwanamitindo Kate Moss; pamoja walisifika mwaka 2005 kutokana na mapenzi yao ya Unga na dawa za kulevya.
Siasa za chama cha Leba (mwaka 1997) zilipitisha sera ya kuruhusu klabu za pombe kufunguliwa saa 24 na hilo limewafanya wananchi kulewa ovyo kila wanapotaka.
Kwetu Afrika wapo baadhi ya wasanii, vijana na wananchi wanaosujudu dawa za kulevya. Hata kama una pesa au wewe maarufu je nini wajibu kwa jamii yako? Wenzetu wanamudu haya kwa kuwa nchi zao zimeshapiga hatua kubwa. Sisi bado tuna safari ndefu. Wapo watakaotetea kwamba nishai hutanzua mawazo. Ukweli nishai haiponyeshi vidonda. Wengine watasema  husaidia utunzi. Kwamba wasanii  waliobadili fani duniani mfano Bob Marley, Jimi Hendrix, Fela Kuti na  walihamasishwa na nishai.
Fela Kuti aliyefariki 1997 kutokana na UKIMWI ni mmoja wa wanamuziki waliohusudu Bangi ingawa alihamasisha na kuwa na ujumbe mkali sana kuhusu maendeleo ya kijamii.

 Lakini je, mbona walifariki wagonjwa sana? Mbona wapo wasanii wengi wanaofanya kazi zao nzuri na kujazia mtungi wa maendeleo bila kutegemea sana nishai hii bandia? Akina Carlos Santana (mpiga gitaa wa Mexico), Mwanarapu Eminem,  Miriam Makeba (mwimbaji wa Afrika Kusini), Gilberto Gil na Caetano Veloso wanaoendelea kutoa mpya mpya, uzeeni,  Brazil. Mifano mingi. Starehe ni sehemu ya maisha yetu wanadamu. Ila inapotegemea usaha hutugeuza kinyesi.  
Ilitoka safu ya "Kalamu Toka London" Mwananchi Jumapili 20, Agosti,2011:
http://www.mwananchi.co.tz/mwananchi-jumapili/43-uchambuzi-na-maoni-mwananchi-jumapili/14697-kutoka-londonkifo-cha-amy-winehouse-fundisho-wa-wabongo

No comments:

Post a Comment