Thursday 20 September 2012

KINYAMKELA CHA MWANAHABARI JULIAN ASSANGE MJINI LONDON



 Niko katikati ya kitongoji cha matajiri, London...
Nimezungukwa na  majumba ya ghorofa, vigae, matofali ya kisasa,  vioo vitupu; mseto wa ujenzi. Punde nimekabiliana na Harrods-  duka maarufu la mamilionea  la ghorofa tano. Harrods imesimama mtaa wa Knightsbridge. Kando yake mna jumba dogo zaidi lenye  matofali rangi kikahawia mtindo wa karne ya kumi na tisa. Mtindo huu unalandana  na mila na desturi za Malkia Victoria aliyetawala karne hiyo (ya juzi) enzi za ukoloni. Nyanyake malkia Elisabeth.

Jengo lina ofisi nyingi na mojawapo ndipo ulipo Ubalozi wa Ecuador. Kawaida Ubalozi mdogo wa Ecuador usingekuwa na haja ya kuandikwa katika safu kama hii. Ila katika kipindi cha miezi miwili – umetajwa tajwa na kufahamika sana.
Hapa niliposimama nje nawaangalia askari zaidi ya kumi wa Kiingereza waliojipanga nje,wakiulinda ubalozi. Upande mwingine wamebana, paparazi na wanahabari na kamera zao; watalii wanapita pita nao wakipiga picha na mkabala wa Ubalozi limejikita kundi la watu, wakipiga kelele, wakiwasuta wale ma-askari. Mmoja wao kashika kipaaza sauti:
“Hakuna mtu aliyepiga simu namba 999 kuulizia msaada wenu, wajinga nyinyi!”
Askari hawasemi kitu. Watasema nini? Nchi hii ina Uhuru wa kusema na kujieleza.  Ukiyatazama mabango waliyobeba waandamaji  na mengine waliyoyabandika kando ya barabara pia mkabala na Ubalozi wa Ecuador, yatakufahamisha nini kinatokea. 
Mathalan:
“Kwanini askari wa Uingereza wanashirikiana na Marekani?”
“Ujasiri Unaambukiza!”
"Chapisheni Ukweli!"

“Uhuru.”
“Ondoeni mikono yenu toka Ecuador!”
“Serikali ya Uingereza ya Aibu lakini si wananchi wake!”
Na mabango kadhaa yana picha za mhusika.
“Mwacheni huru Assange! Msimpige Mjumbe risasi!”
 Yote, yumkini, yanamhusu mwanahabari Julian Assange ambaye toka Juni 19 aliomba ukimbizi  ubalozi wa Ecuador.


 Kisheria, mtu yeyote akiomba hifadhi katika ubalozi wowote na ubalozi ukimkubali, serikali mwenyeji hairuhusiwi kuingilia. Kuingia ndani ya ubalozi ni kukiuka sheria ya kimataifa ya itifaki. Alhamisi 16, Agosti, Ecuador ilimpa Assange hifadhi rasmi. Serikali ya Uingereza ilikataa ikasema itamtia nguvuni. Anashtakiwa kwa kuwanajisi wanawake wawili Sweden na pia Marekani inamtaka asafirishwe kujibu shtaka la hujuma. Akishindwa kesi anaweza kuhukumiwa kifo. 
Ndiyo maana Ubalozi huu wa Ecuador unalindwa na askari wa Kiingereza. Polisi mjini hapa wamesema wazi,  mara Julian Assange atakapotoka tu nje atafungwa pingu. Wiki iliyopita mwanahabari huyu alijokeza nje ya ghorofa ya kwanza akatoa tamko lililopigiwa makofi. Alikanusha madai ya mashtaka ya Waingereza, Waswidi na Wamarekani.
Waliompigia makofi walikuwa marafiki, watu wanaomuunga mkono na baadhi ya wanahabari na mabloga kibao duniani.
Julian Assange ni nani?
Alizaliwa Julai 1971, Australia. Akiwa na umri wa miaka sita wazazi wake walitengana akawa anatanga tanga na mamake. Hadi akiwa na miaka 16 waliishi miji 50 na kuhudhuria shule 37. Haya si maisha ya kawaida. Mwaka 1987 akiwa na miaka 16  alianza kujihusisha na shughuli ya kuharibu mitandao- inayoitwa kwa kimombo “hacking”. Alitiwa nguvuni na wenzake mwaka 1991- na kesi iligharimu dola laki moja. Hakimu alisema angehukumiwa jela miaka 10 kama asingekuwa na maisha ya kuhamahama na ghasia utotoni.
Mmoja wa watetezi wake Julian Assange alimlinganisha na mpigania haki na ukweli, Carl von Ossietzky aliyetunukiwa Zawadi ya Amani ya Nobel (1935) lakini akauawa wakati wa Vita Vikuu vya Pili...

Kati ya 1993 hadi 1999, Julian Assange alihusika na kazi, shughuli mbalimbali za kompyuta na uchunguzi wa siri za mitandao. Mwaka 1997 alichangia uchapishaji wa kitabu kuhusu uharibifu huu(“hacking”) kama mtafiti.  Kati ya 2002 hadi 2005 Assange(tamka “Asanji”)alijiunga na vyuo vikuu vya Melbourne na Canberra kusomea hesabu, fizikia, falsafa na sayansi.Alikatisha masomo yake alipoona wanafunzi wenzake “wakiisaidia serikali ya Marekani kufanya utafiti wa kijasusi.”
Ndipo alipoanzisha tovuti maarufu ya WikiLeaks, mwaka 2006.
Akiwa mhariri wa tovuti hii anasema lengo la WikiLeaks ni kubadili mifumo ya serikali:
“ Lazima tufikirie zaidi ya wale walioshatupita- ili kugundua njia za kubadili teknolojia.” Akaendelea kublogi: “Kawaida mifumo isiyo ya haki huzua wapinzani kufichua madhila yake kusaidia kuwadhoofisha- ili kujenga  mifumo bora zaidi ya uongozi.”
Kuanzia hapo WikiLeaks iliweka wazi madhila ya serikali na makampuni mbalimbali duniani.
Kati ya mambo tovuti hii iliyofichua ni mauaji ya Wakenya wanaopigania haki za binadamu na mawakili, Oscar Kingara na  John Paul Oulo. Wengine wanne waliojaribu kuchunguza mauaji haya nao waliuliwa. Baada ya WikiLeaks kutangaza habari hizi- Julian Assange alizawadiwa Amnesty International Media 2009 Award- ambayo ni tuzo la wanahabari wanaofukua udhalimu wa kijamii.
Baada ya kufichua ufisadi na wizi wa serikali ya Zine Al Abidine Ben Ali wa Tunisia WikiLeaks ilichangia mapinduzi na kuanguka kwake mwaka jana.

WikiLeaks imefichua habari za Bongo pia. Mosi kuhusu mauzo ya shirika la ndege la Tanzania (ATCL) miaka minne iliyopita na namna shirika hili liliponunua ndege mpya kwa njia za upendeleo. Pili, kuhusu mauzo ya rada za Uingereza (BAE) na namna mkuu wa kikosi cha kuzuia rushwa, Edward Hosea alivyolalamika kuogofya atauawa. Malalamiko mengine yalihusu Dk Hosea akisononeka kuwa baadhi ya viongozi Tanzania hawaguswi na mkono wa sheria.
WikiLeaks imefichua sumu na takataka za kimazingira zilizotupwa Ivory Coast, matatizo ya wafungwa wa Kiislamu walioko jela la Guantanamo, Cuba na mengine mengi.
WikiLeaks ilianza kustua zaidi ilipotoa habari kuhusu Marekani na vita. Kwanza ni hati 250,000 za siri za Marekani, kufichua majeshi ya Marekani yalivyoua wananchi Iraq  (Wairaki 11 waliuawa na ndege za Kimarekani, Julai 2007) na Afghanistan(wanawake na watoto 145 waliouliwa na jeshi la Marekani). Habari hizi zilitolewa na askari wa Kimarekani, Bradley Manning, ambaye yuko jela.
Haya na mambo kibao yanayoweza kusomwa zaidi katika tovuti ya WikiLeaks na yameiudhi sana serikali ya Marekani. Ongezea habari za siri za mabenki makubwa makubwa ya Ulaya na habari nyeti za wanadiplomasia mbalimbali duniani.
Yote hayawezi kuenea kuandikwa hapa. Yamemfanya Julian Assange awe mmoja wa wanahabari hatari sana duniani. Si ajabu keshapata tuzo kibao ikiwemo Martha Gellhorn Prize 2010 kwa uchunguzi jasiri wa habari, na hadhi ya mtu muhimu wa dunia iliyoandikwa na jarida marufu la Kimarekani “Time” mwaka juzi. Si ajabu sasa hivi kajificha ubalozi huu wa Ecuador akitafutwa na nyoka na mafahali wa dunia.
Ilichapishwa Mwananchi Jumapili mwezi jana.
Tazama video tuliyotengeneza kuhusiana na suala hapa
  


No comments:

Post a Comment