Monday 17 June 2013

WATOTO WETU WANAVYOANZA KUATHIRIKA NA HALI YA KISIASA NCHINI


Wakati n’naishi Brazili miaka 20 iliyopita moja ya woga mkubwa ulioenea ni hatari ya watoto wadogo mijini. Hatari gani?
Sikiliza ...
Siku moja Jumapili  n’natembea ufukwe maarufu wa Copacabana  jijini Rio De Janeiro. Hapa pana eneo kubwa sana la kuogelea, wanawake warembo, majumba ya starehe, migahawa, magari, minazi na starehe za kuotea tu paukwa pakawa. Jaribu kulinganisha ufukwe huu na Coco Beach , Dar es Salaam. Anzia pale kilima kinachoelekea barabara ya Chake Chake ongoza hadi Kivukoni penye wauza samaki na boti linalovusha watu. Sema badala ya hospitali ya Ocean Road na Ikulu sasa weka majumba hayo niliyozungumzia ya starehe na sehemu ndefu  sana maridadi za kufanya mazoezi na kuogelea.
Watalii walipahusudu. Na hii si yote- ufukwe  wa Copacabana umeunganika na  Ipanema na Leblon, bichi nyingine mashuhuri za jiji. Wabrazili husema Mwenyezi Mungu aliuumba ulimwengu mzima kwa siku sita, ile ya saba akakaa kitako akikamilisha Rio De Janeiro peke yake. Nilikua na tabia ya kwenda kuogelea  na kufanya mazoezi pale mara mbili tatu kwa juma.


 Jumapili hii nilipomaliza  mazoezi na mwanangu tukaelekea kibanda cha madafu. Muuza madafu akatutengenezea mawili- tukasimama pembeni na mrija tunafaidi maji  ya bahari Atlantic.
Ghafla  kundi la watoto kama sita saba hivi, hilo. Kisa nini ? Wamemwona mtoto mwenzao. Wastani wao miaka sita, saba, minane. Hawa watoto lakini hawakua wa kawaida. Ni watoto yatima wanalala na kuishi mitaroni na vijiweni; wametupwa au hawana wazazi, wametoroka majumbani,  hawana pa kwenda.
Kwa kuwa nilishakaa kipindi  jijini nilijua lengo la wale vifaranga nini. Haraka haraka kabla mambo hayajageuka kokoto- maana mwanangu alikua akianza kuwayowayoka- nikawanunulia madafu. Wakanywa.
Sasa umefika wakati wa kuondoa kile wala madafu tunachokiita “nyama” yaani nazi changa ambayo huwa tamu na madini tosha. Mchonga madafu keshatutayarishia, sasa tunayala na kijiti kile kile kilicho sehemu ya mnazi. Kwa mla madafu ada na desturi.
Punde, hilooo... kundi la watalii. Watalii wabichi- ukiwachunguza wanavyotembea, bwede bwede bwe, hawajakaa sana mjini. Mosi hawaijui lugha- maana ikiwa huongei Kireno hapa Brazili- umejichongea, ni sawa na kutojua Kiswahili kwetu Afrika Mashariki. Watoto walipowasikia wale “Gringos” (wageni wanavyoitwa) wakiongea Kispanyola cha kubabaisha na Kiingereza, wakawaparamia.
Mtoto wa kwanza - miaka saba hivi- mtemi, ndiyo kiongozi.
Kaanza kwa Kireno: “Tunaomba madafu ba’ mkubwa!”
Mtalii kamwangalia mtoto, kisha  wenzake, inavyoelekea neno lililotambulika moja tu: “agua de coco”( madafu).
Mtalii akamjuza  mwenzie Kiingereza : “Hawa si wale watoto wa siku ile?”
“Ndiyo hawa hawa ...” akahakikishiwa.
“Pesa imekwisha.” Akasema mtalii kiongozi.
“Pesa imekwisha?” mtoto kiongozi miaka saba  akajibu; midomo imefyodolewa, anawakagua wageni utosini hadi miguu iliyovalia kandambili za bichi; kinda wa mitaroni, hata panya hamthubutu. Sasa nimeshajua nini kitafuata; nikampa ishara mwanangu. Tukaondoka  tukasimama kama mita hamsini pembeni, tukimalizia “nyama.”
Mungu akikupa kilema hukupa na mwendo.
Kiongozi yule wa miaka saba kaingiza mkono tumboni chini ya fulana yake chafu (tumboni!), akachomoa bastola. Akawaelekeza  watalii. Madafu yamesahauliwa; vifaranga  wamewazunguka, wanadai dhahabu. Muuza madafu tu ndiye kabaki akitafadhalisha kwa Kireno:
“Tulizeni mambo vijana” (hakusema watoto, ila vijana! Mguu wa kuku ni Ustaadh).
Watalii wamenywea utadhani mbunge maarufu aliyefumaniwa. Mifuko imefunguliwa, fedha zimetolewa, watoto haoooo... wakatoweka na chao. Haukupita muda lakini wakatiwa mbaroni.
 Enzi nikiishi Brazili ilikuwa kawaida kusikia watoto wa aina ile wameuawa na polisi.
Julai 1993,  watoto wanane waliuawa na watu ambao baada ya uchunguzi kufanywa –  walikisiwa kuwa maaskari, mjini Rio. Moja ya utetezi walioufanya ni kusema eti wanasaidia kufagia (kusafisha) mji kutokana na adha ya watoto wanaohalifu na kuchafua jiji.  Wastani wa watoto waliofyekwa ulikua miaka 11 na 14. Katika taarifa ya polisi na mahakama baadaye, baadhi ya  walionusurika walisema asubuhi hiyo (ya mauaji) walikuwa nje ya kanisa la kikatoliki liitwalo Candelaria. Gari la polisi liliwapita na mmoja wao akawapigia kelele: “Msijali tutawakomoa siku moja!”
Kati ya walionusurika-  Sandro do Nascimento- alikuja kuwa maarufu sana alipoteka nyara basi kitongoji cha Rio kiitwacho Jardim Botanico  mwaka 2000. Tukio lilisababisha kiwewe  na kutangazwa runingani  siku nzima. Leo unaweza kulitazama katika sinema: Bus 174, ambayo toka itolewe  2002 imeshinda tuzo 23 duniani. Sinema hii muhimu  inatathmini hali halisi ya watoto wa maskini,  yatima na hatima zao.
Kwanini nimeeleza kisa?
Wakati  nikiwa Brazil, watoto  waliua na kuuliwa;  waliogopwa na kuchukiwa – kielelezo cha  jamii iliyochechemea.
Madhila  ya Brazil yametokana na ukosefu wa elimu hasa kwa hohehahe na yameenea nchi zinazoendelea. Sinema nyingi karibuni zimeonyesha namna  watoto hugeuzwa askari jeshi  Uganda, Sierra Leone na Liberia.   Ingawa bado hatujafikia  kiwango hicho  taratibu hali ina dalili  za kidonda, Tanzania.
Karibuni matukio mawili muafaka yameongelewa sana mtandaoni. La kwanza ni mabanda ya kuonyesha video  mijini. Malalamishi yaliyoenea ni kwamba ingawa  vimepigwa marufuku na serikali- bado utawakuta watoto wa shule wakiingia vibandani  usiku kutazama  filamu za ngono,  ambazo si za  umri wao. Matokeo, anaandika mwananchi mmoja, kuna kesi nyingi za watoto wadogo kuwaingilia ( kuwabaka) wenzao kimwili.  Mwananchi anacholalamika ni serikali na chama tawala kutotekeleza tamko la kupiga marufuku vibanda husika. Kaiita mada na ombi lake : “Udhaifu wa serikali na mmomonyoko wa maadili mitaani.”
N’nakumbuka mwaka mmoja uliopita nilipotembelea nyumbani nilikua katika basi Dodoma kuelekea Arusha nikashuhudia sinema ambazo zilikuwa na mwelekeo wa watu wazima zikionyeshwa ilhali ndani ya basi walijazana watoto.
Tukio la pili ni watoto wetu wanaoishi mpakani Kenya na Tanzania kutoroka mashuleni kufanya kazi za kuajiriwa na kuuza bidhaa Kenya. Hii ni kutokana na kile mwandishi  alichokiita “kufanya vizuri kwa thamani ya fedha ya Kenya kuliko ya Tanzania.”
Iko mifano mingi; lakini hii miwili ni inadhihirisha  maadili na maisha ya wanafunzi wetu  kudhoofika. Hatujaongelea kutofaulu mitihani.
Dalili za mvua ni mawingu. Kwa sasa haya  ni madogo , lakini tusipozima moto unaoanza kuunguza maadili, watoto  wetu  kushika bunduki halitakua jambo la ajabu siku za usoni.

 Ilitoka pia Mwananchi Jumapili




No comments:

Post a Comment