Thursday 13 February 2014

WAALIMU NA WAHADHIRI WANALO JUKUMU KUBWA KUENDELEZA ELIMU AFRIKA


Kufuatana na kampuni maarufu ya huduma za uhasibu, Ernst na Young, yenye makao makuu London, kuanzia mwaka 2,000 hadi 2015,  Afrika iko katika maendeleo makubwa  kiuchumi. Ingawa sisi wenyewe tunajihisi hali mbaya, ulimwengu mzima unalitegemea bara  kwa mali asili na hali ya hewa.
Na hayakuanza leo. Baada ya mkutano maarufu wa Berlin ,  1884- chini ya uenyekiti wa Mfalme Otto Von Bismarck- wakoloni walikuja, wakaondoka.  Watawala wenyeji wakaendeleza uzi ule ule wa kikoloni: kupora; wakishirikiana na wakubwa; wakihadaa kwa maneno maneno na bunduki. Dunia nzima inatushangaa vipi, sisi matajiri wa mali ghafi, bado tunategemea misaada; vita vya wenyewe kwa wenyewe, magaidi wanaua hadi wanafunzi na watoto : Nigeria. Wanawake wanabakwa, Kongo, Sudan na Jamhuri ya Afrika ya Kati.  Kwa maskini asiye na mali au nguvu za kisiasa, elimu tu ndiyo ubwabwa uliosalia.  
Asili mia ndogo sana wanafikia shahada ya mwanzo  (Bachelors) au  Diploma; na  kidogo zaidi kuendelea shahada ya kati (Masters), uzamili.
Kama Francis Magomeni(jina la bandia) aliyekuja kusoma shahada ya uzamili (uchumi), London, karibuni.
“Nataka niwe kama akina Profesa Lipumba, Profesa Palagamba Kabudi,  Profesa Muhongo. Si lazima niwe Waziri, lakini niwe fresh.  Nchi yetu yahitaji wataalamu.  Wakenya, Uganda, Burundi wanachukua kazi zote, kwa vile sisi hatujasoma.”

Hayati Nyerere. Mwanaelimu na mwalimu maarufu kuzidi wote katika historia ya Tanzania.
Picha ya Wikipedia....


Changamoto, changamoto.
Alinigusa zaidi alipotaja suala la waalimu na wahadhiri wetu.
“Waalimu hapa Ulaya tofauti kabisa na nyumbani. Wanachapa kazi. Hawana makuu, wala kujidai dai.  Kuna siku nilipewa kazi, lakini kutokana na presha za maisha, nikababaisha babaisha nikampa tu mwalimu, nikidhani atamezea. Lakini mmh. Nilipomlalamikia akatingisha kichwa.  Hakutaka kuongea zaidi. Nikasimama pale nikisubiri, ah wapi. Nimezoea nyumbani. Waalimu, wako kinamna. Anaweza kukupasisha au kukuchukia tu, akakufelisha.”
Kwanini akuchukie?
“Ah linaweza kuwa jambo la kipumbavu kama labda una gari zuri, yeye hana. Au wewe ni demu kakuomba mchezo ukamkatalia. Au labda unapiga piga sana makelele darasani, kila saa katika simu. Jambo kubwa au dogo, ili mradi waalimu kule kwetu wanaweza kukuharibia maisha,  makusudi.”
Tofauti na huyu Mzungu wa London ilikuwa ipi?
“ Baada ya kumsimamia pale nikimsubiri, akaniuliza kama nimesoma alichokiandika chini kabisa ya karatasi zangu. Kumbe mimi na Uswahili wangu, sikuwa nimesoma. Nikatazama nikakuta maneno mazito sana. Akasema, sikujibu maswali. Na vitabu vinne nilivyotakiwa kuvitafuta na uchunguzi niliotakiwa sikuufanya.  Akaniamuru niende tena maktaba, kuchimba. Hakuwa na kosa. Miye ndiye niliyelipua. Nimezoea nyumbani. Mwalimu anaweza kukufanyia kila aina ya hila; fanya vizuri, ufanye vibaya.”
Hii si mara ya kwanza kusikia malalamishi ya aina hii. Je, kweli waalimu wetu nyumbani wanafanya watakavyo? Francis Magomeni:
“Kwanza,  tabia. Nimeshakaa hapa miezi mitano. Nimechunguza.  Huyu jamaa niliyemsema ni profesa. Ukimwona njiani huwezi amini.  Anafika, anafundisha, anasahihisha; anatoa orodha ya maswali, anaelekeza vitabu, anaondoka zake. Ukifanya vizuri unapewa maksi za kufaulu, ukifanya vibaya unanyimwa, lakini unapewa sababu. Huwezi kumhonga au kufanya usanii. Utamwanzaje?”
Sasa kinachotisha, kimoja.
Itakuwaje waalimu wetu waitwe “wafidhuli”   ilhali takwimu zinatueleza mengine?
 Wakati TANU ikidai Uhuru miaka 60 iliyopita, idadi ya waalimu ilikuwa ndogo sana, na Mwalimu Nyerere mwenyewe alikuwa kati ya wachache. Mwaka 1970,  elimu kwa wote (UPE) ilikuwa asilimia 100. Ilipofika mwaka 1974 wakati namaliza kidato cha sita; Azimio la Musoma, liliwapa wanafunzi wa kike kipaumbele. Kawaida baada ya kidato cha sita tulitakiwa kwenda jeshini miezi 12, na kuajiriwa miaka miwili kabla ya kuendelea chuo kikuu. Sera ya Musoma iliwapa fursa wasichana waendelee moja kwa moja. Kutokana na azimio hilo la kimaendeleo, leo tunao akina mama wanataaluma wa kujivunia  baadhi  viongozi kama Dokta Asha Rose Migiro, mwanadiplomasia Mwanaidi Maajar (aliyekuwa Balozi Uingereza na Marekani), Balozi Radhia Msuya (Afrika Kusini) na hata Waziri Profesa Anna Tubaijuka (ingawa yeye alisoma kabla ya sera hii).  Baada ya vita vya kumwondoa Idi Amin, 1979, uchumi ulipoanza kuanguka, idadi ya waliosoma ilidondoka. Kitwakimu, tunaambiwa na mtaalamu wa Haki-Elimu, Rakesh Rajani,  mwaka 2000, “Idadi ya watoto walioandikishwa iliporomoka hadi asilimia 77. Utafiti ulionyesha takriban zaidi ya nusu ya watoto wote walikuwa hawamalizi shule ya msingi, ambapo waliotoka familia fukara ndiyo wengi. Ubora wa elimu ambao haukuwa wa kuridhisha tangu awali ulizidi kushuka kufikia moja ya viwango vya chini duniani.”
Mwanauchumi Francis Magomeni anatujuza:
“Kutokana na hali ngumu ya elimu nyumbani,  waalimu wana nguvu ya masultani. N’na dada yangu fulani tulimaliza naye chuo kikuu , 2008. Aliendelea na kazi ‘afu,  akaanza kusomea diploma ya utawala; mimi nikawa natafuta vyuo vya nje. Ananiambia hasomi kwa amani. Waalimu vijana  wanawaandama wasichana.  Anasema hakuna siku inayopita bila kutongozwa.  Ukikataa unafelishwa.”
Je, hawa waalimu wanazingiatia maadili na kanuni za kufundisha? Francis Magomeni akacheka:
“ Kweli hayo ya huku hayapo nyumbani. Kila siku tunasoma katika magazeti ya Uingereza namna mwalimu kafukuzwa kazi au kapelekwa jela kwa kutongoza  au kulala na mwanafunzi. Juzi hapa si kuna yule mwalimu mwanamke aliyetangazwa  kalala na mwanafunzi wa miaka 17? Wakakutwa wakifanya ngono ndani ya gari? Si ameachishwa kazi? Nyumbani, nyoo. Mpaka mtu atangazwe gazetini? Hutokea ndiyo lakini nadra; ukilinganisha na mamia ya waalimu wasiokuwa na zile adabu na heshima, nyinyi wenzetu mlizopitia enzi za Nyerere. Huyu sista ananieleza waalimu kutongoza wanafunzi wa kike imekuwa nongwa kiasi ambacho wasichana  wanadhani  ukisoma unatongozwa na mwalimu! Usipotongozwa  si kawaida! Shule zimekuwa sehemu za ukahaba? Wasichana watasoma wawe kama akina Profesa Tubaijuka na Dokta Migiro kweli?”
Duu.
Magomeni alikuwa akipandisha jazba.
“Waalimu wa huku si noma. Anafanya kazi yake, anaondoka.  Halafu nimechunguza jambo moja kubwa sana. Watu wa huku hawajifaragui na elimu. Unamkuta mtu ana udokta au uprofesa, lakini hakwambii wala haweki cheo mbele. ”
Nikatafakari aliyosema Bwana Magomeni. Nikawazua kuhusu taaluma zinazotegemewa na mwananchi mitaani.   Askari asipotulinda,  tutaishi kwa amani kweli? Dereva akilewa au kuvuta bangi kazini, si hatari kwa abiria? Je, mganga akikosea kumpa mgonjwa dawa, si kifo? Mwalimu ni mzazi wa pili wa mtoto. Kama walivyo waganga, madereva, wanausalama, mwalimu ana jukumu kubwa sana !

No comments:

Post a Comment