Friday 4 April 2014

MWANAMKE WA LONDON ALIYEOANA NA MBWA ANATUKUMBUSHA NINI?

Amanda Rodgers akimbusu mbwa aliyefunga naye ndoa. Picha ya Medavia

                  

Majuma mawili yaliyopita habari za mwanamke wa London aliyeoana na mbwa wake aitwaye Sheba zilitangazwa  na gazeti la Metro. Metro hutolewa bure,  kila siku, kwa wasafiri miji mbalimbali ya Uingereza. Baadaye Bi. Amanda Rodgers alipohojiwa na  ITV mjini London alidai : “Nafahamu ndoa yangu na Sheba haitambuliki kisheria. Lakini ilikuwa njia nzuri ya kuonyesha ninavyomthamini Sheba. Sheba amekuwa nami miaka mingi, hunichekesha na kunifariji ninaposononeka.  Sikuweza kumpata mwenzi mwingine wa maisha kama huyu.”
Huyo ni Mbwa  anayeongelewa, babu eh.
Mwenzenu alishachoka, aisee.


 Baada ya kuishi na wanaume wawili, kuyeyushwa na mahusiano na kero akaamua. Aaakheri mbwa. Tena tunakosea hapa tunapomwita mwenzie, mbwa. Mila ya wafuga mbwa wa ndani( kinyume na walinda nyumba,  wanaosaidiana na polisi nk) ni kuwa nao kama sehemu ya familia, kuwatunza na kuwapa majina mithili ya ndugu yeyote wa damu. Hivyo Sheba (ambaye ni mbwa jike) alitimiza kanuni za mapenzi ambazo mwanamke huyu mwenye umri wa miaka 47 alizihitaji.
Kwani siri ya mapenzi ni nini, huuliza wanasaikolojia?
Niambie msomaji. Siri ya fenesi la moyo nini?
Wimbo mmoja wa Taarabu uliwahi kushauri zamani : “Ukipenda Pendeka...”
Amanda Rodgers keshaishi miaka 47, ndiyo.
Miaka arobaini na kitu kwa mwanadamu huitwa “umri wa makamo” kwa Kiswahili.  Bado uzee kushtadi hakika,  bali kukomaa kimaisha; kupitia mengi hata ikibidi kujaaliwa kajukuu.  Lakini si wote tunaojaaliwa haya...
Hapa Uzunguni ndoa zimefikia kilele cha ugumu siku hizi. (Ugumu kiasi ambacho ndoa za jinsia moja zinapigiwa madebe kukidhi haja...!)
Kihistoria, miaka 50 sasa  Uhuru na Ukombozi wa akina mama umeleta maendeleo katika uchaguzi wa kazi na taaluma,  mahusino na wanaume, malezi ya wanao, kujiamini na kujituma, nk. Hapo hapo maendeleo haya yameporomoka kiuwiano. Wanawake wamekuwa wahitaji na wakali zaidi, na matokeo ndoa hazidumu. Wanaume wanakimbia majumbani.  Habari za baadhi ya midume kuzaa kisha  kuua watoto, mke na wao wenyewe zinazidi kuenea. Wanaoumia ni watoto.
  Katika hali hii “ngumu” unawakuta  wachache wanaoamua bora kuoana na viumbe wengine kuliko wana-Adam.
Kuna habari za waliooana na nyoka, samaki, hata waliofunga ndoa  na “vitu” walivyovihusudu mathalan, madaraja, viwanja vya kuchezea nk. Yanachekesha, yanastaajabisha, yanakondesha,  yanasikitisha.
Ila mahusiano mazuri kati ya mtu na mbwa ndiyo mbingu.
Mbwa ni kiumbe anayethaminiwa sana Uzunguni. Nakumbuka mara yangu ya kwanza kuzozana na utamaduni huu nilikuwa naishi Ujerumani mwaka 1985.  Mmoja wa jirani zangu alikuwa na mbwa mwenye tabia mbili zilizoudhi sana. Kwanza hubweka usiku na mchana kutokana na kufungiwa ndani na kuhasiwa. Wazungu huwahasi wanyama  kuzuia kuzaa zaa ovyo. Hii ni kutokana na uhaba wa nafasi majumbani, ukosefu wa muda wa kuwahudumia(shughuli na kazi nyingi) na gharama.  Huku Uzunguni huwezi kumrushia mbwa wa jirani kipande cha mfupa au masazo ya chakula ovyo ovyo. Hairuhusiwi. Vile vile mwenye mnyama  hatokubali.  Vyakula maalum vya wanyama huuzwa madukani na  masupamaketi.
 Tatizo la pili ni hulka. Kiasilia, wanyama huishi maporini. Maisha ya mijini yenye kelele za magari, lami,  uchafu wa moshi na viwanda, nk si  makini kwao. Ongeza sasa hizo nafasi ndogo za kufungiwa ndani, mbwa hukosa jaha. Wanaojiweza huajiri “watembeza mbwa”(dog-walkers)  wanaotoza fedha kwa waliokwenda kazini (kwa kukosa nafasi) kuwatembeza na kuwafanyisha mazoezi.
Hilo, moja.
La pili, mbwa huyo wa jirani aliacha kinyesi chake pale mlangoni kwangu. Kila nilipolalamika  n’lionekana eti nimejaza tu chuki.  Ilitokea hata siku moja mgeni wangu akakanyaga kinyesi cha uharo.  Zingatia harufu iliyokithiri na matusi yaliyotutoka.
Nilipogomba nikaambiwa : “Ah nyinyi Waafrika mnachukia wanyama, mnatesa wanyama, hamna utamaduni wa elimu viumbe!”
Baada ya malalamiko ya majuma kadhaa, kutosikilizwa na kupuuzwa, nikaamua sasa kumvizia yule jibwa. Asubuhi moja wakati akijisetiri mlangoni nikamvizia na tofali dogo (maana mawe hayapatikani ovyo miji ya Ulaya) nikambabua vizuri. Kilio alichokitoa kilizagaa mithili ya kinyamchela eneo lote lile. Magari yalisimama. Wapita njia wakaduwaa. Utadhani nimeua.  Pamoja na yale mavi kuwa ushahidi nikaandamwa. Simu ikapigwa polisi. Dakika kumi hazikupita, king’ora hicho. Askari watatu wakaja; pingu mkononi, vigongo. Nikazolewa mkuku hadi kituoni.
“Akili zako ziko sawasawa?”
Nikaelezea hali mbaya ya kinyesi na kadhalika.
“Kwanini hukuja kituoni kushtaki?”
Nikasema sikujua kama unatakiwa  kumshtaki mbwa kwa kwenda haja kubwa.
“Unatakiwa ndiyo. Huo ni uchafu wa mazingira.”
Yote yalikuwa mapya kwangu. N’lizoea mengine, Afrika.
“Umefanya kosa la jinai. Umemdhuru kiumbe na mali ya mtu.”
Maneno yalikuwa mengi. Lakini pamoja na ukali wao,  sheria za nchi hizi zina haki. Ukishtakiwa unapewa pia wakili. Wakili akatetea sijaishi sana nchini. Nimezoea mazingira na utaratibu mwingine bara Afrika. Sifahamu utaratibu, nk
Nikaonywa.  Lakini ilibidi kuhama; kila nilipopita nilinyoshewa vidole kitongojini. Kampiga mbwa. Mtesa wanyama, nk.
Mbwa, paka na wanyama, kijumla huheshimiwa sana. Na si ajabu kwamba huyu Bi Amanda Rodgers akaamua kufunga nao pingu za kheri. Ukitazama video au sinema zinazoonyeshwa katika mtandao wa “You Tube” utathibisha mahusiano haya. Taswira za wanaume kwa wanawake wakipigana mabusu (midomoni) na mbwa ni nyingi sana. 
Kijana wa miaka 19 , Wayne Bryson, alifikishwa mahakamani mapema mwezi huu kwa kufanya ngono na mbwa wa mke wake. Mke  anasema asingefahamu kilichokuwa kikiendelea kama si jamaa kujipiga picha ya video katika simu yake.
Kisa kilichojulikana zaidi duniani ni  cha dada wa Kimarekani, Alyssa Rosales aliyefanya ngono na mbwa kwa  takriban dakika moja halafu akasambaza video Facebook na You Tube. Baada ya malalamishi iliondolewa. Leo Alyssa katajirika kutokana na tendo hili. Ukitaka kuitazama filamu pana malipo.
Lakini si Wazungu tu.
Video za Wakongo, Wakorea na Wachina wakichinja mbwa, kuwauza au kuwala kama kuku zimejazana  You Tube.
Yote haya yanatueleza nini kuhusu maisha yetu ?
Je, mapya?
Sidhani.  Toka zamani wanadamu tulikuwa na tabia ya “kufanya vitendo” na wanyama. Leo vyaonekana zaidi kutokana na uwazi na  usambazaji haraka wa habari. Vile vile siku hizi wanadamu hatuoni aibu kuelezea mambo yetu ya undani, hadharani. Ni sura halisi ya maendeleo tuliyoyafikia.















                    

No comments:

Post a Comment