Sunday 30 November 2014

VITA DHIDI YA KULAWITI NA KUBAKA WATOTO VYAWAKA MOTO UZUNGUNI – Sehemu ya 2





Vitendo viwili vichafu  “vinavyofichwa” na watawala duniani ni biashara ya dawa za kulevya na unyanyasaji wa watoto. Ingawa  vya aibu na ufidhuli vina faida sana kwa wahusika. Dawa za kulevya ni biashara inayotajirisha haraka kuliko zote.
Ripoti iliyotolewa na Idara ya Kuzuia Uhalifu na Dawa za Kulevya ya Umoja wa Mataifa (UNIDOP) mwaka 2011, inasisitiza  asilimia 20 ya  kipato cha dunia hutokana na biashara hii ya ki-Ibilis. Ndiyo maana mtu yeyote anapopambana na ujambazi huu lazima atauawa. Haya yanaonekana Mexico - kilele cha ujambazi wa dawa za kulevya. Video za mauaji – wakiwepo wanawake na vigoli- wakikatwa katwa  kwa mapanga, visu na mashoka zimeselelea mitandaoni.
 Habari za Watanzania waliokamatwa wakibeba unga au “heroin” ughaibuni sasa zimekuwa nongwa.
Unyanyasaji wa watoto hauna faida ya kiuchumi ila ni “jaha” kwa wahusika.  Hali kadhalika ni rahisi kuwatumia watoto  kubeba silaha, mizigo, kuwalawiti nk. 

 
Wiki hizi mbili zilizopita Uingereza imeshuhudia  sokomoko la wakuu wa nchi walivyofanya  kila njia kuzuia habari za ngono na watoto kutofichuliwa.
Madai  yalifanywa na mmoja wa vizito  ndani ya serikali ya chama cha Conservative kati ya 1979 na 1990.  Inadaiwa  mafaili yaliyotayarishwa  na marehemu  Geoffrey Dickens  mwaka 1983 yaliharibiwa  baada ya kufikishwa polisi.  Uongozi wa sasa wa Waziri Mkuu, David Cameroon umethibitisha kuwepo kwa mafaili 746,000,  ofisi za Wizara ya Mambo ya Ndani kati ya1979 na 1999.  Miongoni ya hayo 114 yaliyoharibiwa, 13 yanahusu uchunguzi wa unyanyasaji wa watoto. Neno linalosikika ni “paedophilia”- yaani tabia ya mtu mzima kuhusudu mapenzi au ngono na watoto.
Bado madai yanaendelea kujadiliwa serikalini.  Dai muhimu lasema viongozi wa ngazi za juu, wakiwepo wanadini na familia ya malkia walihusika. Aliyekuwa madarakani wakati huo ambaye sasa hivi ni mstahiwa mwenye hadhi ya “Lord” ...anadaiwa alimbaka mwanafunzi wa miaka 19 mwaka 1967.
Kidesturi wadhifa wa “Lord” unatokana na umwinyi Uingereza na familia ya wafalme. Leo mtu yeyote aliyefanya mazito jamiini anaweza kuteuliwa kuwa Lodi.  Wanawake huitwa Baroness. Mfano ni Mjamaika, Baroness Doreen Lawrence ambaye mwanae, Stephen, aliuliwa na wabaguzi wa Kizungu, London, mwaka 1993. Baroness Lawrence amepigania haki ya mwanae kirefu hadi kuwapeleka baadhi ya wahusika jela.
 Moja ya manufaa ya “Malodi” (neno lililoshaingia ndani ya msamiati wa Kiswanglish) huruhusiwa kuingia kikao maalum cha Wabunge. Kikao kina nguvu za kupitisha miswaada na sheria za serikali.
  Tuendelee.
 Dai la pili la kashfa hii inayoitetemesha Uingereza- linasema  uongozi wa enzi za marehemu Margaret Thatcher ulijaribu vile vile kubatilisha sheria za kuruhusu watoto chini ya umri wa miaka 16 kufanya ngono.  Wiki jana kamati ya uchunguzi ilitahadharishwa kutoficha baadhi ya madai ikiwepo jina la askofu maarufu aliyelawiti watoto.
Haya mambo yapo kila mahali.
  Lakini hayasemwi. Kwetu Tanzania- miaka mingi- tabia ya watu wazima au  wenye nafasi kubwa kulala na watoto imeenea. Chawa  ameanza kuonekana karibuni kutokana na mjadala kuhusu ushoga.
Miaka mitatu sasa serikali za Kizungu –zikiongozwa na Wamarekani zimetutaka Waafrika kulegeza sheria za mapenzi ya jinsia moja. Kinyume na namna mahusiano haya yanavyokuwa nchi zilizoendelea, ushoga, kwetu si utamaduni na wale wanaofanya huwa wamelazimika.
Mtafiti na mchunguzi  aliyetuma makala ya kurasa tatu ndani ya moja ya mitandao  jamii inayosomwa na Waswahili.  Anadai:
“Sidhani Marekani inatutaka tukubali ushoga. Ni kunyanyasa na kuonea ndiyo inataka tuache maana...hawa tunawatengeneza wenyewe kwa kulawiti vitoto... watu wenye mahitaji tunatumia ngono kama chombo.”
Nakubaliana na mwandishi. Zamani nikisoma shule za kulala za sekondari  ilikuwa kawaida baadhi ya wavulana kufanywa wanawake kwa nguvu na vijana wakubwa zaidi. Wapo waliopigana na  walioshindwa. Walioshindwa waligeuka mashoga. Mmoja niliyesoma naye Mzumbe mathalan ( vitendo viliitwa “umbuzi”), alikuja kuwa shoga maarufu.
Si mashuleni tu. Mtafiti anaendelea kusema “Malezi ya nyumbani –kulaza watoto wadogo wa kiume na wakubwa wanaonea wadogo kisha wanazoea – kwa asilimia 80. Mlinzi, dereva wa watoto, mtoto wa kazi za nyumbani analawiti wanao- wewe mwajiri hujui, dereva humfungi maisha unamfukuza kazi; unapokuja kufahamu mwanao keshazoea. Humsaki aliyemfanya hivyo. Hausigeli anasaga vitoto au wadogo zake.”
Ni mambo yanayotokea majumbani, kisirisiri, tunayafahamu; hatuyapingi.
Mwandishi anaelezea utafiti aliofanya  Dar es Salaam kuhusu ulawiti. Anadai  siku hizi ili kupata ajira, kinachotakiwa si fedha bali ngono: “ Kwa changu doa kipato ni kikubwa zaidi asipotumia Kondom au akikubali Tigo.Wafanyao haya ni waume za watu, waheshimiwa, watu wa dini, wenye hela, makampuni, hoteli – wenye vipato. Wasichana wanahadaiwa,  hatimaye wanaharibika.”
 Mbali na ulawiti unaoendelea mitaani, mashuleni na katika taasisi za kidini (mathalan madrassa) mtafiti anagusia tatizo la homoni. Homoni au “hormones” kwa Kiingereza ni viini vinavyoendesha mizunguko na tabia za maumbile. Watu wanaogeuka jinsia zao kutokana na kulawitiwa wakiwa wadogo au ujanani kihomoni ni wengi Tanzania anadai mchunguzi.
“Zamani wazee wa mila walikuwa wakiwavunja lakini siku hizi tunawaficha hatuna mila za kikabila tunazozifuata na kuwasaidia. Hospitali ni gharama. Aibu. Mbona wapo wanaume wenye viuongo vya kike na kiume na wameoa?”
Madai mazito.
Suluhisho nini?
Vyombo vyetu vya habari bado havithubutu kujadili. Bado tunajificha katika shuka za mila na desturi. Wanaoumia ni watoto na watu wazima walioharibiwa vijijini na mijini.
Misaada ijayo kupitia taasisi na vyama mafichoni haiwafikii, inaliwa na wachache bila kuwapa huduma ya hospitali na ajira.
Halafu vipi mtu aliyelawiti au kuharibu watoto anapokamatwa mbona ndugu zake humtolea dhamana na kumnyanyasa mtoto au kijana aliyebakwa?
 Kwanini tunaruhusu hawa watesaji kutembea majiani huku tukiwanyanyasa walioharibiwa na kugeuzwa mashoga?Viongozi wetu hasa Wabunge  wanapashwa kupitisha sheria kali kuwatia nguvuni wanaoharibu watoto.  Lakini je serikali yetu iko tayari kufukua handaki na shimo hili la kiza?













No comments:

Post a Comment