Sunday 7 June 2015

URASTA SI BANGI, UKAIDI, UCHAFU, UHUNI WALA UJAMBAZI



Ethiopia imeelea ndani ya habari za kimataifa  wiki hizi mbili.
Jumapili iliyopita wanawake watatu  wa Kihabeshi  walishinda  mbio za Marathon hapa London. Zilishirikisha wakimbiaji 38,000, wengi  wananchi wa kawaida ( wasio  wanariadha wa kulipwa);  mataifa mbalimbali. Baada ya ushindi “ wanariadha hawa wenye fahari” walipeperusha bendera rangi kijani, manjano na nyekundu. Bendera hii ya Ethiopia iliyosanifiwa mwaka 1897  imekuwa  kielelezo maarufu cha Umoja wa Waafrika na watu weusi duniani zaidi ya miaka mia moja sasa.  Wekundu ni nguvu na imani, kijani ardhi na manjano, kanisa. Tufasili hili kifupi.


 Mwanamuziki maarufu wa Reggae kutoka Ivory Coast, Alpha Blondy. Picha ya Reggae Ville.

Ethiopia na Liberia ndiyo mataifa pekee Afrika ambayo hayakutawaliwa na Wazungu au Waarabu. Sifa na fahari hii iliwapa motisha watu weusi waliochukuliwa  utumwa Ughaibuni na kuiita Ethiopia (Abyssinia) taifa la Wafalme. Kanisa (rangi njano ya bendera) lina historia ndefu Ethiopia. Ingawa  mna madhebehu mengine, Ukristo umejizatiti Ethiopia toka karne ya kwanza. Kabla hata ukoloni haujabuniwa au Uislamu kukanyaga barani.
Wiki mbili zilizopita Wahabeshi 30 waliuawa na magaidi  wa ISIS shauri ni Wakristo. Akilaumu mauaji hayo yaliyofanyika Libya, Papa Mtakatifu Francis, alimtumia salamu  mkuu wa kanisa la Tewahedo, Abuna Matthias. Kanisa hilo ndilo lenye wafuasi wengi Ethiopia.
Tukio la tatu lililowakumba Wahabeshi tulilitaja juma lililopita. Kati ya maelfu ya wakimbizi waliotaabika bahari ya Mediterranean walikuwepo  raia wa Ethiopia. Taifa hili la kale halikutawaliwa na wageni shauri jeshi lake la kifalme lina zaidi ya karne 20 sasa. Sifa hii ndiyo ilichangia kuanzishwa  makao makuu ya Waafrika mjini Addis Ababa mwaka 1963. Umoja  ulifanikishwa na viongozi Kwame Nkrumah (Ghana) Mwalimu Nyerere (Tanzania), Kenneth Kaunda (Zambia), Ben Bella (Algeria), Ahmed Sekou Toure (Guinea) na Mfalme Haile Sellasie (Ethiopia). Bahati mbaya leo ukitafiti maandishi mengi wanaotajwa ni Nkrumah na Haile Sellasie tu. Yabidi kizazi kipya kifahamu historia ya kweli.
Tufukue zaidi.
Hadhi ya Ethiopia na  bendera ya Ethiopia ndizo zinazojulikana kama rangi za Rasta.
Aliyeongoza msisimko huu ni kiongozi wa watu weusi, Marcus Garvey. Marcus Garvey alisisitiza imani ya kuupenda Uafrika nchini Marekani, visiwa vya Karibian na Uingereza. Bw Garvey aliyezaliwa Jamaica mwaka 1897, alikuwa mwanahabari, mfanya biashara, mchapishaji vitabu na mzungumzaji mzuri. Alianzisha chama cha kuwarejesha watu weusi Afrika kwa meli aliyoiita Black Star. Kwa miaka hiyo ya 1920 – 1940 alikuwa jasiri na mwanamapinduzi thabiti aliyewasisimua viongozi tosha mathalan, Jomo Kenyatta, Kwame Nkrumah, Malcolm X, Nelson Mandela, nk.  Baada ya mapambano makali, alihamia London alipofariki 1940 akiwa na miaka 52. Athari ya kazi ya Marcus Garvey ni kubwa sana katika historia na harakati za watu weusi.
Enzi Marcus Garvey akipigania haki hizi, kundi la Wajamaika walioipenda na kuiheshimu Ethiopia lilianzisha dini ya Rastafari mwaka 1930.  “Ras” ni kichwa (au aliyeteuliwa) kwa Kimhariki (lugha ya Kihabeshi).  Kimaudhui ni mfalme au mtoto wa mfalme. “Tafari” inatokana na “Tefar” ambayo kwa  Ki- Amhariki ni “anayeogopewa”, au “kustahiwa”...Urasta pia hutumia neno “Jah” toka  Jehovah – Mungu kwa   Kiebrania, lugha ya Wayahudi.  Marasta wanaamini Haile Sellassie anatokana na damu ya Yesu Kristo; mrithi wa kizazi hicho.
Fikra za Marcus Garvey na Urastafari  vilipewa uzito na muziki wa Reggae, ukiongozwa na bendi maarufu ya The Wailers. Bendi iliasisiwa mwaka 1963 na Peter Tosh (aliyefariki 1987), Bunny Wailer (yungali hai) na Bob Marley (fariki 1981).  Reggae ilichanganya imani ya Rastafari (kutukuza Uafrika), mafundisho ya Marcus Gavey (  muungano wa Waafrika) na harakati za walala hoi.
 Mahadhi ya Reggae na Rasta  yalitukuzwa na masharti rasmi mfano kutokula nyama, kusoma Biblia,kutokata nywele,  mazoezi ya mwili, amani, nidhamu na kuvuta jani (herb) liitwalo bhang (Kihindi), marijuana (Kispanyola, tamka marihuana) na  spleef (Kijamaika, tamka splif).
Si kila mfuasi wa dini ya Rastafari huvuta bangi. Mutabaruka, mshairi mashuhuri wa Reggae (asiyevaa viatu, asilani) havuti bangi, hanywi pombe, hali nyama. Mjamaika, Mutabaruka hutumbuiza kwa muziki,   redio na duka lake la vyakula vya afya.
Zaidi ya miaka arobaini sasa Urastafari umezagaa duniani. Mbali na wanamuziki, yapo mambo ya kifani mathalan namna Marasta wa Kijamaika walivyobadili nywele za msokoto (“locks”) kwa kupachika neno “dread”  yaani “kuhofia” jambo fulani.
“Dreadlocks” ni nahau inayoendeleza mapigano ya Marasta na ukombozi dhidi ya mateso ya maskini, wanaoonewa na  weusi duniani. Kwetu Uswahilini hutumia neno “nywele za rasta”  kufasiri (au elezea) mtindo. Ukweli “kusokota nywele” si jambo jipya.  Nywele za mtu mweusi kiasilia zimejisokota, na zisipochanwa, zikiwa ndefu hugeuka “kuwa Rasta.”
 Mau Mau wa Kenya, waliopigana dhidi ya wakoloni wa Kiingereza kati ya 1952 hadi 1956, aliponyongwa kiongozi wao shupavu, Dedan Kimathi, walikuwa na nywele hizi. Walichofanya wanamuziki wa Reggae na Marasta ni kutukumbusha tu  asili yetu. Urasta  si dawa za kulevya, au wenda wazimu.  Mtanzania unapoacha nywele chafu, huku ukivuta bangi na kufanya mizaha inayowatisha au kuwahasimu wanajamii wenzako, kama kutukana wazee katika mabasi au kukaba usiku, hufuati  Urastafari. Urastafari  ni ukombozi, kujitambua, kujipenda, elimu na maendeleo ya jamii.
Tupeane mfano muafaka?
Mchimbe mwanamuziki  maarufu wa Reggae, Ivory Coast, Alpha Blondy. Karibuni kaanzisha kituo cha redio mjini Abidjan. Malengo ya “Radio Alpha Blondy FM, 97.9” ni  kutumbuiza muziki wa Reggae na vichekesho, kutoa ajira, na kuhimiza kusoma vitabu.
Kila juma, Alpha Blondy husoma kitabu kilichoandikwa na Mwafrika.
 Alipohojiwa na runinga ya Ufaransa, TV5, mwezi  Machi,  Alpha Blondy (aliyeingia uwanja wa muziki mwaka 1982 na kibao, Brigadier Sabari) alisisitiza hana malengo ya kisiasa :
 “Kuna mtu aliwahi kuandika ukitaka kumficha mtu mweusi habari iweke ndani ya kitabu. Sababu sisi  weusi hatupendi kusoma. Nimeamua kutumia redio sababu kinyume na runinga ambayo ni ya kutazama, inakubidi kusikiliza na kuzingatia maneno. Azma yangu ni kujenga mapenzi ya lugha, fasihi  na vitabu.”
 Hii ni ithibati adhimu ya Urasta na hulka zake. Ikiwa unaendekeza bangi, matusi hadharani, kupiga watu, kupora  na utovu wa nidhamu; ndugu yangu Mwafrika, tafakari na tafiti zaidi.

  
-Ilichapishwa Mwananchi Jumapili, Mei 3, 2015.



No comments:

Post a Comment