Friday 6 November 2015

KWANINI WASTANI WA MAUTI YA MTU MWEUSI ALIYESOMA NI MIAKA 55-65?




Mwandishi nikiwa na mtunzi mashuhuri hayati Gil Scott Heron (kushoto), baada ya onesho lake Jazz Cafe, London.  Scott- Heron alifariki akiwa na umri wa 63, mwaka 2011. Picha ya A. Macha , 1999.


Nilikuwa naongea na rafiki yangu mhadhiri; Dk Ikaweba Bunting, anafundisha  Marekani...
 Tulisononeka kifo cha mshairi maarufu wa mahadhi ya Jazz, marehemu Gil Scott Heron. Bw Scott Heron alikuwa na ujumbe mzito uliotetea maslahi ya wananchi weusi wa Marekani na kuzungumzia matatizo kadhaa ya jamii hiyo ukiwemo utumiaji dawa za kulevya. Alipiga piano na kuandika riwaya na mashairi matamu na makali sana. Ukitaka mfano mzuri hebu tafuta “Pieces of a Man” katika You Tube. Sikiliza sauti yake mshairi anayesemwa kuwa ni  baba wa watenzi wa Rapu na Ushairi wenye ujumbe. Fuatilia piano iliyotulia na mdundo  wa Blues na Jazz. Kama unahusudu lugha,  zingatia namna Kiingereza kinavyotumiwa kumchora na kumhakiki mhusika anayeimbwa.  Hayati Gil Scott Heron aliandika riwaya na kufundisha fasihi.  Anaomboleza maisha ya mtu huyu aliyeanza na bangi huishia  jehanam. Baadaye jamaa anateketea kabisa.
“I saw him go to pieces.
He was always such a good, good man.”
(Nilimtazama akivunjika vipande vipande
Alikuwa mtu mzuri sana...)



 Niliwahi kumhoji marehemu Gil Scott Heron mara mbili.  Kila nilipokuwa naye nilijifunza mengi kuhusu utunzi, fasihi, wajibu wa raia kwa jamii zao na mapenzi ya maisha. Kama mwanamuziki nilikumbushwa uzuri wa kutumia ala na vyombo kuelezea kadhia. Sasa tuliposikia Bw Heron kafariki akiwa na umri mbichi wa miaka 62, mwaka 2011, tuliduwaa.
“Kwanini watu weusi , hasa wanaume tunafariki umri huu?”
Tukaulizana maswali mengi...miye na  Dk. Ikaweba Bunting.
Inakuwaje?
Hukwe Zawose , nguli wa muziki wa jadi toka Tanzania alifariki  na miaka 63,  Desemba 2003. Hadi leo ukilitaja jina la Zawose huku Majuu waliomjua, wakiwemo wasanii wa Kiafrika, wasanii na wananchi wa Kizungu hutingisha vichwa.
 Mara yangu ya mwisho kukutana na Zawose ilikuwa hapa London alipokuja na mpwa wake, (pia marehemu), Charles Zawose mwaka 1996. Hukwe alitumbuiza na Salif Kaita , albino na mwanamuziki maarufu wa Mali ukumbi wa Barbican Centre.
Ukumbi bab kubwa.
Peke yake,  Zawose ( na Ilimba na zana nyingine Kigogo) alitingisha dimba, utadhani kapandwa na radi, kageuka tsunami, sauti nyororo inayobadilika badilika kuwa kisu, rungu, upinde na mawimbi. Akafa na miaka hiyo, 63.
Mwandishi nikiwa na hayati Hukwe Zawose, alipokuja kutumbuiza ukumbi maarufu wa Barbican Centre. Picha ya Les Rickford, 1996

Mwanamuziki mashuhuri wa Kimarekani aliyefariki mwaka 1991 na miaka 65 alikuwa mpiga tarumbeta wa Jazz, Miles Davis. Miles Davis hakuwa tu mwanamuziki shupavu aliyechora picha wakati wake wa mapumziko. Miles alileta mapinduzi katika fani hii ya Jazz kwa kuibadili mara nne. Kwa vipi?
Wakati Jazz ilipoanza karne ya 20 ilikwenda haraka na “wababe wake” walikuwa Louis “Satchmo” Amstrong (tarumbeta na kuimba), Duke Ellington (Piano), Dizzie Gillepsie (Tarumbeta) na  Charlie Parker (Saxafoni). Hadi leo hakuna mpiga Saxafoni anayemfikia Charlie Parker kwa kwenda haraka. Baada ya kupiga na bendi ya Parker kwa kipindi (akiwa bado anasoma) Miles Davis aliamua kubadili mwendo.
 Miles na tarumbeta yake. Picha ya jalada la kitabu cha maisha yake na F Macha, 2015.

 Alituliza muziki wa Jazz kuwa wa taratibu zaidi.
 Huo ndiyo mwanzo wa “Cool Jazz” unayoisikia  sana katika mahoteli makubwa na sehemu za tafrija za mapenzi na familia, duniani.  Miles alichagua wanamuziki wazuri kuzidi wote akawaingiza katika bendi zake. Chini yake aliwapa moyo na mafunzo. Wote wamekuwa wanamuziki wakubwa. Mfano ni Herbie Hancock na mpiga besi mashuhuri  Marcus Miller.
Tatu, Miles alichanganya Jazz na miziki ya kisasa enzi alizoishi na kuunda mseto unaoitwa Fusion Music.  Alikuwa mvumbuzi na hakupenda kujirudia rudia aliloshalifanya. Vyuo mbalimbali duniani hutumia miziki yake kunoa nadharia ...Mathalan kusisitiza “ukimya” katika muziki. Kwamba “ukimya”  ni muhimu kama ilivyo “kelele.” Mpiga gitaa mashuhuri Carlos Santana kakiri hadharani kafunzwa sana na nadharia hii.
 Mwanamuziki Remmy Ongala aliyefariki mwaka 2010 akiwa na umri wa miaka 63. Picha ya Jack Vartoogian, New York, 1989...
Mwingine ni Fela Kuti, mwanamuziki mwa Nigeria.
Fela Kuti alisomea Jazz hapa London. Aliporudi kwao alitumia ujuzi alioupata kufufua jadi la kabila lake la Kiyoruba; akaunda mapigo ya “Afro Beat.” Leo Afro Beat imekuwa mtindo mashuhuri.
 Wanawe wawili, Seun Kuti na Femi Kuti wanaendeleza sanaa ya baba yao aliyeingia jukwaani na wake zake 30. Aliwaita “malkia zangu”...
Fela aliwahi kusema katika mahojiano kuwa wanaume wengi huwa na wanawake pembeni -yaani nyumba ndogo. Wanaficha. Yeye huwaweka wote hadharani ili kila mtu ajue. Ukosefu wake huo wa unafiki, ulimponza. Mbali ya muziki wa Afro Beat alishika ujumbe mzito uliowaudhi mafisadi serikalini.
 Mwaka 1977 wanajeshi waliingia  eneo lake aliloliita “Jamhuri ya Kalikuta” wakampiga yeye, wake zake na kumtupa mama yake mzazi toka ghorofa ya pili. Mama Fela alifariki baadaye kutokana na majeraha ya tukio.
Msanii Kuti  alifariki mwaka 1997 akiwa na miaka 58.
Wanahabari waliotutoka karibuni Tanzania ni pamoja na Mike Sikawa ( miaka 55, mwaka 2008), Adam Lusekelo (miaka 56, mwaka 2011)...Mhadhiri mpendwa Profesa Chachage S Chachage alifariki 2006 akiwa miaka 51. Chachage ni wa rika langu. Tulisoma wote na tulifanya  michezo na mazoezi tukiwa Mzumbe. Baadaye bahati mbaya Chachage aliacha kufanya mazoezi...
Chachage (aliyenyoosha ngumi mwanzo) ...tukiwa pamoja Mzumbe katika timu ya ndondi shuleni. Picha ya Harold Mhando, 1974.

Hii ni mifano michache ya wanaume mashuhuri weusi.
Ni kitu gani kinachomfanya mtu mweusi asiendelee zaidi ya  65? Ndiyo wapo wachache wanaosonga mbele lakini kwanini matarakimu huwa  wastani huu zaidi?
Labda msomaji unayo majibu.
Kitabu kipya cha hayati Chachage kilichotoka 2014. Mkusanyiko wa makala zake mbalimbali. Kimechapwa na E & D Limited, Dar es Salaam. Picha ya F Macha, 2015
Kwa tathimini yangu naweza kuwaangalia hawa niliowataja juu.
 Sababu ya kwanza iliyowakumba  ilikuwa ulevi na dawa za kulevya. Ulevi kupindukia husababisha kisukari. Na kisukari husababisha kifo. Vijana wengi duniani hupenda  kuvuta bangi. Unapotumia bangi hatimaye utataka vikali zaidi. Matokeo huharibu mapafu, ubongo nk. Miles Davis alikiri katika kitabu cha maisha yake (Miles, 1989) kuwa dawa za kulevya zilichangia kuharibu mahusiano  na familia yake.
Ya pili ni maradhi ya ngono kama UKIMWI.
Hili huwafika watu mashuhuri kutokana na maingiliano yao kirahisi na wanadamu wengine. Kukosa nidhamu, kutoangalia hatari ya matokeo ya unachokifanya ni kati ya majanga. Na kwetu sote tuliobakia tujifunze nini?
Kila kifo kinapotokea huwa huzuni. Huwa wakati wa kumwomba Mungu atunusuru. Wakati mgumu. Wakati huo huo ni vizuri tukaanza kuchunguza nini sababu zinazotufanya wataalamu weusi kufariki mapema zaidi, hasa pale sababu zinapoweza kuzuilika.



Ilichapishwa pia Mwananchi Jumapili katika gazeti taslimu, Novemba Mosi 2015....

No comments:

Post a Comment