Sunday 3 January 2016

BARUA YA WAZI KWA RAIS MAGUFULI KUTOKOMEZA KABISA UKEKETAJI TANZANIA





 Mpendwa Rais John Magufuli,

Kwanza nakutakia kheri za mwaka mpya wa 2016.
 Ninakupongeza kwa kuanza kazi yako kwa kishindo. Kishindo kinachowapa wananchi wetu matumaini. Mvumo unaoukupa sifa Afrika Mashariki nzima hadi kuwafanya wenzetu watuonee wivu.  Afrika nzima inatamani ingekuwa na viongozi kama wewe. Tunaoishi Ughaibuni tutaendelea kuwa mabalozi wako.
Leo mada yangu Mheshimiwa Rais ni suala la ukeketaji.
Wasichana waliokimbia kujihifadhi jumba la Mugumu, Mara. Picha ya Anthony Mayunga kupitia gazeti la Mwananchi.

 Wiki jana gazeti la Mwananchi  lilitoa habari kuhusu kituo kipya cha hifadhi ya wasichana wilayani Tarime,  kinachosimamiwa na kanisa la Kikatoliki Mara. Toka Novemba 15 , wasichana 2,118 walijisalimisha hapa kukwepa ghasi na hari ya ukeketaji wa ukoo wa Warenchoka.
Kituo kilijengwa kwa jitihada za wananchi Mara na wafadhili mbalimbali huku Uingereza waliochanga fedha na wanaoendelea kuushutumu ukeketaji.  Waliosimamia ukusanyaji wa fedha hizi walikuwa wana Jumuiya ya urafiki baina  Uingereza na Tanzania (British Tanzania Society).
Nikiwa  mmoja wa Watanzania  nilishiriki katika kampeni za kukusanya fedha nikipiga muziki wa ngoma. Niliandika pia makala kadhaa kuchangia suala. Hivyo,  nimefuatilia kimbunga muda mrefu.
Katibu  wa kituo hiki cha kuwahifadhi wasichana wanaotoroka ukeketaji, Bw Dickson Joseph aliitaka “sheria ya makosa ya kujamiiana ipewe meno na serikali ili kufanyiwa kazi.” Hili ni ombi muhimu sana Mheshimiwa Rais.
Bi Rhobi Samwelly toka Mara akihutubia kikao cha kiserikali Uingereza kilichotayarishwa na BTS (Jumuiya ya Urafiki Uingereza na Tanzania), kuhusu ukeketaji na wananchi wanavyoshughulika.

Kwa vipi?
Baadhi ya wasichana  waliohojiwa na mwanahabari Mwaitara Meng’anyi walidai wanapokimbia au kuukwepa ukeketaji wanakanwa na jamii.  Ndugu na vyombo mbalimbali  huwakosesha elimu. Ilidaiwa msichana  mmoja aliwahi kuwa mgonjwa wa akili kutokana na hilo. Je taifa lisilosomesha wasichana ni taifa gani, Mheshimiwa Rais?
Wahudhuriaji wa mkutano wa kushutumu ukeketaji katika ukumbi wa Central Hall, Westminster, Novemba 2014.



Kati ya juhudi na malengo ya hifadhi kama hii si tu kuwakimu wasichana hawa zaidi ya 2,000 waliokimbia adha, bali kuwahudumia kwa elimu, maarifa na ujuzi mbalimbali. Hata hivyo bado haijulikani kama watarejea kwao wakimaliza. Je wazazi na ndugu watawakubali?
Ukumbi wa The Russet,  London ukitumbuizwa kwa mashairi na muziki, kukusanya fedha za ujenzi wa jumba la Mugumu, Oktoba 2014.

Mbali na hilo, Mheshimiwa Rais Magufuli, ikumbukwe jumba la hifadhi kama hili- ni moja tu. Bado kuna mamilioni ya wasichana nchini kwetu ( na penginepo) ambao hawatapata fursa ya kutoroka. Takwimu zilizotolewa na shirika la kimataifa linalofuatilia ukeketaji duniani “"FGM 28 Too Many” hapa Uingereza lilidai mwaka jana kuwa ni mikoa ya Zanzibar na Mtwara tu isiyo na ukeketaji.
Mwandishi nikiwa na Anna Marie, Mkurugenzi wa FGM 28 Too Many

Mikoa inayoongoza ni Arusha, Manyara, Singida, Dodoma ikifuatiwa na Mara, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro. Wanaoendeleza desturi mara nyingi ni maskini vijijini. Wananchi ambao huenda hata wasisome barua hii au kusikia tunalolisema hapa. Asilimia 80 ya Watanzania.  Wengi ni  wanawake. Wachapa kazi.
Bango la kukemea ukeketaji ndani ya gari moshi la London mwaka 2014.

Mheshimiwa Rais wewe ni mchapa kazi na umehimiza sera ya “Sasa Kazi”....Zamani mwasisi wa taifa letu, hayati Mwalimu Kambarage Nyerere aliwahi kusema yafuatayo kuhusu wanawake mashambani:
“Itakuwa vizuri kuwauliza wakulima, hasa wanaume, ni saa ngapi kwa juma au majuma mangapi kwa mwaka wanafanya kazi? Ukweli wanawake vijijni hufanya kazi sana, saa 12- 15 kwa siku. Hufanya kazi pia Jumapili na siku za sikukuu. Wanawake wanaoishi vijijini hufanya kazi zaidi ya mtu yeyote mwingine Tanzania. Lakini wanaume vijijini huwa likizo nusu ya maisha yao.”


Mwalimu Nyerere na ngoma ya mgambo. Picha ya Getty

Kifupi, waathiriwa ukeketaji ni wachapa jembe vijijini. Sheria lazima iwalinde na si tu iwalinde kwa maneno bali kwa vitendo. Haya yamesemwa mara nyingi na viongozi waliopita. Mwenyewe Mwalimu Nyerere na mkewe Mama Maria Nyerere walishutumu sana ukeketaji. Mwezi April 2015 mkutano wa kitaifa uliofanyika siku mbili hoteli ya Kunduchi , Dar es Salaam, ulikemea ukeketaji. Akihutubia viongozi mbalimbali wa dini, sheria, kanda na serikali, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Bi. Sophia Simba alisema baadhi ya makabila yanaondeleza mila za kuwakeketa wanawake na watoto ni “ukatili mkubwa unaoleta madhara ya kiafya” na kusababisha vifo, vilema na  magonjwa kama fistula.  
Mganga kuu wa wanawake waliokeketwa, London, Dk Comfort Momoh, toka Nigeria akihutubia kikao cha Wabunge wa Uingereza na wanachama wa Jumuiya ya Uingereza - BTS mwaka 2014.

Wazungumzaji wengi ndani ya mkutano huo walipinga vikali ukeketaji na kumtaka kila mtu kujiunga na upinzani wa mila hii muflis.
Lakini je, utekelezaji wa shutuma na kauli ukoje?
Je watu wangapi wameshtakiwa? Je mbona bado wasichana wa Tarime waliohojiwa juzi na mwanahabari Meng’anyi walikuwa  na hofu? Je wasichana wengine Tanzania wasiopata fursa ya kuhojiwa (au kupigwa picha na vyombo vya habari) kama hawa wa Tarime huishia wapi?
Ukweli tatizo hili si letu tu.
Mataifa ya Kizungu pia yamekuwa yakipambana na kukinzana na ukeketaji. Shirika la Afya duniani (WHO) linakisia nchi 28 za Kiafrika na Mashariki ya Kati (Yemen, Saudi Arabia, Misri nk) zinaendeleza ukeketaji. WHO inakisia kati ya wanawake na wasichana milioni 100  hadi 140 wamekeketwa.  Kila mwaka milioni mia tatu wanakatwa – kitakwimu ni 8,000 kwa siku, WHO inadai.
Mtanzania mkazi Uingereza, Peter Mwita toka Mara, akitoa hoja katika kikao cha kushutumu ukeketaji Uingereza. Bw Mita alisema anafahamu watu wake na kwamba kinachotakiwa ni elimu vijijini. Desturi imepitwa na wakati, alisisitiza.


Janet Chapman na Jonathan Pace wa kitengo cha misaada (Tanzania Trust Fund) UIngereza kilichopigana kutafuta fedha kujenga na kumalizia kituo cha Mugumu.

Kutokana na hilo serikali za Uingereza na Ufaransa zenye wahamiaji wengi Ulaya, zimepitisha sheria kali. Uingereza mathalan ilipitisha sheria kuzuia ukeketaji mwaka 1985 na kuiboresha 2003. Hata hivyo baada ya miaka yote hiyo ni mwaka 2014 ambapo wahusikawa kwanza  walishtakiwa. Mganga, Dk  Dhanuson Dharmasena (31) na  mzazi Hassan Mohammed (40) walidaiwa kutibu au kufanya ukeketaji. Serikali ilikiri waziwazi kuwa ni vigumu kuwashtaki w ahusika shauri jamii huficha na kuendeleza desturi hii kisirisiri. Hapo hapo...
Mbunge wa chama tawala cha Uingereza, Conservatives, Jeremy Lefroy aliyeshutumu ukeketaji. Picha ya BBC

Ufaransa  ilikuwa na kesi 100, mwaka 2014. Watoto wa kike, Ufaransa, hutazamwa, kukaguliwa na kuangaliwa na mahospitali hadi wanapotimiza miaka sita.
Swali hapa Mheshimiwa Rais ni utekelezaji wa sheria. Akitoa moja ya masuluhisho mwaka jana. Kaimu Mkurugenzi Mkuu shirika la Kimataifa la kuhudumia watoto -UNICEF Geeta Rao Gupta alimtaka kila mwanaume, mwanamke, mzee kwa kijana kushutumu ukeketaji kwa nguvu. Hilo mosi.
La pili, Mheshimiwa Rais ni wewe mwenyewe kuendelea kulitaja kama moja ya madhara makubwa kwa uhai wetu.

Mama Balozi Uingereza Joyce Kallaghe akiwa na Rhobi Samwelly na mwenyekiti wa Jumuiya ya kina mama Uingereza, Mariam Kilumanga. Pamoja kushutumu Ukeketaji
Kwanini?
Kwanza kama tulivyoona juu kina mama vijijini ni wazalishaji mali na wachapa kazi wanaotegemewa na jamii kiuchumi na kijinsia. Pili wanawake ndiyo wanaotegemewa  kuendeleza vizazi vyetu kama wazazi. Ikiwa tunaharibu kisima hiki , je maji tutayatoa wapi? Si kama kujinyima silaha ya uhai, Amiri Jeshi wetu Mkuu?

 Mwandishi na kundi lake la Kitoto wakitumbuiza ukumbi kwa Ngoma katika kikao cha Westminster Hall.

Makala ilichapishwa pia gazeti la Mwananchi Jumapili, 3 Januari 2016.





No comments:

Post a Comment