Thursday 16 June 2016

TUJIFUNZE NINI TOKA MAISHA NA HEKAYA ZA MUHAMMAD ALI ?



Bondia Muhammad Ali alipotembelea Tanzania mwaka 1980 akiwakilisha Marekani kuhusu michuano ya Olimpiki Moscow iliyokuwa na ukinzani. Kushoto kwake ni Thomas Mweuka wa Ofisi ya Habari Marekani Tanzania, USIS. Picha ya Mtandaoni.


Mwanadamu anapofariki huacha mali, watoto au maarifa. Mengi  yameandikwa ( na yataendelea kusemwa) kuhusu maisha ya bondia maarufu  Muhammad Ali aliyezikwa Alhamisi, Kentucky, Marekani.
  Wapo watu mashuhuri aina mbili.

 Waliofahamika kwa kitendo au vitendo fulani na waliobadili kabisa mambo au mitazamo.   Ali yumo kundi la pili.  Mifano michache ni  Wagiriki Aristotle, Pluto, Socrates au Mjerumani Karl Marx aliyesasambua fikra za kikomunisti .   Yesu Kristo,  Buddha na  Mtume Muhammad SAW, hawana ufafanuzi. Mwanasayansi Albert Einstein alivumbua nadharia ya bomu la nuklia. Wanasiasa kama Mahtama Gandhi, Abraham Lincoln na Fidel Castro ( bado hai) wa Cuba. Afrika tunaye Mtemi Shaka Zulu,  Nelson Mandela na Mwalimu Nyerere aliyejitahidi  kuunda jamii mpya. Michezo? Pele wa Brazil, mwanariadha Jesse Owens aliyewika miaka 80 iliyopita. Na Muhammad Ali.
Kwanini Ali yumo?
 Tumgawe mafungu manne. Taaluma , maarifa , msimamo na udhaifu.
 Kitaaluma Ali alianza  ubondia akiwa na miaka 12...baada ya kudhamiria kulipiza kisasi jamaa aliyemwibia baiskeli yake. Zamani mabondia waliingia tu kilingeni , hawakusema sema, walituna madita tayari kuchapana. Kwa watu weusi Marekani masumbwi yalikuwa ajira iliyotajirisha. Ali alibadili kabisa mtazamo huo wa kuwaona mabondia mbu-mbu-mbu!!! Aliifanya taaluma ya kustarehesha na kupendeza. Kiufundi alipiga kichwani tu. Hakuendekeza desturi ya mabondia kurusha ngumi “popote tu” mwilini. Na akipiga sehemu fulani ataidonoa pale pale hadi ipasuke, ivimbe au kutota damu. Ufundi huo anao chui. Simba, duma au mbweha humkamata mnyama shingoni , mkiani au popote pengine. Lakini chui akivizia hushika sehemu moja. Habadili badili hadi nyama imegeuka kitoweo. Neno la Kiingereza ni “stealth”....Hila na werevu.
 Ali alikuwa na wepesi wa kila kitu : miguu, mikono na mwili usiotulia.  Kwa wanamasumbwi wa uzito wa juu si rahisi kuruka ruka na kucheza densi. Mbwembwe zake zilichanganya kukwepa haraka akienda  kinyume kinyume na kiupande upande kama kaa baharini. Aliita mtindo wake sayansi. Si ajabu mpiganaji maarufu Bruce Lee alimwiga. Ukitazama sinema ya “Enter The Dragon” utaona sanaa za Ali kwa Mchina huyu ambaye wengine (nikiwemo) tunamhusudu kuzidi chapati na fenesi.
Maarifa.

Ali miaka ya Sitini, akifanya masihara na watoto mitaani...

Kidesturi wanamichezo si watu wanaowekwa kundi la wanafikra. Ali alitabiri lini atamtumbua mpinzani wake, na juu  alitongoa mashairi na kuunda misemo lukuki; yenye falsafa, ucheshi, sanaa na majigambo ya kisakolojia.
 Nina spidi kali. Jana usiku nilizima taa nikawahi kufika kitandani kabla chumba hakijapata giza.”
Au utashi wa nahau na fasihi:
Nimepigana mieleka na mamba, nikabingirishana na nyangumi,nikautia umeme  pingu: na kuifunga radi jela.  Wiki iliyopita niliua jabali, nikajeruhi jiwe, nikalitia tofali hospitali. Mimi mkali  huzifanya dawa ziugue.”
Aliwasanifu aliopigana nao ili kuwapiku kiakili...
Alimwita Sonny Liston “dubu” , Joe Frazier “gorila” na kumtania George Foreman ( Congo- Zaire, 1974) kiasi ambacho leo Foreman hucheka akikumbuka: “Kila nilipompiga ngumi, Ali alificha uso nyuma ya mikono yake akinisanifu, Joji ni hicho tu ulichonacho? Na ukweli  nilishamaliza nguvu zote. Ha ha ha.”
PIcha maarufu ni ile ya Ali alipomchapa Sonny Liston aliyekuwa akiogopewa mwaka 1963. Hata hivyo watu hawakuamini ngumi aliyomwangusha nayo ilikuwa kweli. Ilibidi pambano lirudiwe na ukweli ukabainika. Picha ya Mtandaoni.

Enzi hizo George Foreman na Sonny Liston waliogopewa kama Mike Tyson alivyokuja kuwa.  Kabla ya pambano waganga walishatayarisha gari ya kumbeba Ali kumkimbiza hospitali. Aliwazidi.
 Funzo kwetu hapa ni kutumia akili na saikolojia kupambana na maisha. Ali hakusoma na kipimo cha Wazungu cha akili yake ( IQ) kilimpa namba78 ambayo ni chini sana. Hiyo inatuelezea nini kuhusu mizani za Wazungu na uwezo wa mwanadamu?
Tatu.
Msimamo wa Ali.
 Watu weusi waliteswa na kudhalilishwa kwa neno: “nigger”....Wakati Ali akianza kupigana miaka ya  Hamsini, weusi walikuwa  wakinyongwa hadharani na Wazungu. Hivyo  michezo  na sanaa ilikuwa tegemeo kuu la kujiendeleza.
Baada ya kushinda medali ya dhahabu (Olimpiki, Roma, 1960) na kuwatangwa mabondia zaidi ya 20, akiwemo Sonny Liston,  Ali alibadili jina la Cassius Clay kuwa Muhammad Ali mwaka 1964. Dini ya Kiislamu kwa weusi Marekani kipindi hicho ilikuwa dini ya kimapinduzi. Hata leo Waislamu weusi wamejenga jamii zao zenye nidhamu na kutofuata mienendo iliyowekwa na Weupe. Kila alipoanza pambano alionekana akiinama na kusali. Alikuwa na nidhamu na alisema yeye mzuri, akiwa na maana watu weusi wazuri na shupavu.
 Alikataa kupigana vita vya uenevu Vietnam. Ukitazama sinema ya Ali (aliyocheza Will Smith, 2002), utashuhudia pale Ali anapotoka mahamakani  akishutumu serikali na kusema yuko radhi kwenda jela kuliko kusafiri mbali kuua watu ambao hawajahi kumdhalilisha.  Anachotaka ni uhuru. Huu ni uanaharakati wa hali ya juu. Walimvua taji lake la ubingwa  1967 hadi 1970.
“Huduma kwa wengine ni kodi tunayotakiwa kulipa kwa chumba tulichopewa hapa duniani,” alidai.
Funzo kwetu  ni kuwa na msimamo thabiti,  kutotetereshwa  na mali, uongo au vitu. Ali aligeuza taaluma yake kuwa chombo cha kuwakomboa watu wake kutoka utumwani. Kila alipoweza aliitaja Afrika ambapo mabondia wa leo kama Floyd “Money” Mayweather wanadharau. Ali alitembela Tanzania mwaka 1980.
Udhaifu.
Ali alioa mara nne. Kati ya wanawe tisa, Laila Ali, binti,  ndiyo aliyemrithi ubondia na hadi alipojiuzulu 2007 hakupigwa. Mke wa mwisho Lonnie alijitolea kumuuguza na kusimamia mali zake. Inadaiwa  mtoto wake pekee wa kiume Ali Junior yuko katika hali mbaya  kimaisha. Kabla ya mazishi, habari kwamba dola milioni 55 alizoacha Ali  tayari zimeanza kugombaniwa zimezagaa magazetini.
 Ali akiwa na binti yake Bondia Laila,  aliyepigana hadi 2007 bila kushindwa. Picha ya Mtandaoni



 Mganga na kocha wake Ali, Ferdie Pacheco, alimwonya mwaka 1975. Hii ni  baada ya pambano kali kati yake na Joe Frazier,  lililoitwa “Thriller in Manila.”  Lilichukua raundi 15 na Joe Frazier alilazwa hospitali.  Dk Pacheco anasema Ali alipokataa kujiuzulu, aliachana naye. Kuanzia hapo Ali aliendelea kupigana hadi 1981. Akapatwa na maradhi ya Parkinson mwaka 1984. Ugonjwa wa Parkisons hushambulia ubongo.
 Funzo hapa ni mwanadamu  kujua kikomo cha nguvu na udhaifu wako. Kusikiliza ushauri na kutokuwa mwenye tamaa. Utunzaji wa mali, kuhakikisha tunaacha wosia unaofaa na familia.
 Mwanamuziki maarufu, Bob Marley, alieacha watoto kumi na moja alikataa kuacha karatasi ya mirathi. Suala lilichukua miaka kumi kusuluhishwa mahakamani. Mjane wake, Rita Marley, ndiye anayesimamia mali hiyo iliyokuwa dola milioni 30, leo ni 130 milioni. Rita amewakubali watoto wote Bob aliowazaa na wanawake saba , na kuhakikisha hawadhaliliki.

-London,  8 Juni , 2016
-Barua pepe: gmacha52@gmail.com

No comments:

Post a Comment